Mtangazaji wa Kipindi cha Ala za Roho, Loveness Love maarufu kama Divathebawse ambaye siku chache zilizopita aliweka wazi juu ya tatizo lake la mirija ya uzazi kuziba hali iliyopelekea kwa kipindi kirefu kushindwa kupata mtoto amesema tayari amefanya taratibu zote za kupata mtoto na anatarajia kupata watoto watatu na tayari amepata mbegu za mwanaume huko nchini Uturuki.

”Sio kwamba nakuwa na mtoto na mwanaume ambaye nina mahusiano naye ananipa tu sperm zake zinaunganishwa na zangu napata mtoto, nilicheki Uturuki, Japan na Marekani nikaona Uturuki bei yao ni nafuu Zaidi, niliongea na daktari nikamwambia sina mahusino lakini nahitaji mtoto atakuwa wangu ningependa nipate mtoto wa Kitanzania lakini hapa nchini hakuna sperm bank” amesema Diva.

Hadi hivi sasa amechangiwa kiasi cha pesa Shilingi Milioni tano kupitia Instagram na kusema kuwa hakutegemea upendo huo ulioneshwa na watanzania kwani tayari anaona ndoto yake ya kupata mtoto inakaribia kutimia na ameshafanya mawasiliano na daktari wa kumfanyia taratibu hizo za kumpandikizia mbegu.

“Hadi sasa hivi zimepatikana milioni tano waliochanga kupitia instagram, wadau waliokuwa nje ya nchi wamenitumia akina mama kutoka kampuni moja ya simu, sijategemea upendo walionionyesha Watanzania, wamekuwa wakinipigia simu, wengine wanasema kuna dawa wanataka kunipa za kuzibua mirija na kiweza kuzaa kwa njia ya kawaida lakini nimeshatumia sana dawa ni tatizo nililoumwa kwa muda mrefu, kwahiyo nimeona ili tuzipoteze tena hela za madawa ni bora kusafiri nje ya nchi kwenda kufanya hicho kipimo cha IVF.

Hata hivyo mtangazaji huo hakusita kutoa shukrani zake kwa uongozi wa Clouds Media na boss wake Sheba Kusaga, kwa kuwa naye katika kipindi hiki cha mpito ambacho wamekuwa wafariji wakubwa na kumuahidi kuwa kila kitu kitakuwa sawa na atapata mtoto wake mwenyewe , ”tena sio mmoja hata wawili au watatu” ameongezea Diva.

Aidha Diva amesema ameamua kutumia njia ya IVF yaani ya upandikizaji mbegu kutokana na kwamba tayari amefanya vipimo vyote na kwa kuwa tatizo hili ni la muda mrefu haoni haja ya kuendelea kupoteza hela kununua dawa ambazo ametumia kwa muda mrefu bila mafanikio.

”Nimeshaumwa sana tumbo kwa muda mrefu, niliambiwa ninaweza kupata mtoto kwa njia ya kawaida lakini itakuwa kama ni maajabu ya Mungu ndivyo alivyosema daktari, lakini ili niwe na uhakika ni bora ni save ili nitumie njia ya IVF, sasa hivi nimeanza kuwa na matumaini ya kupata mtoto”.

Pia ametumia nafasi hiyo kutoa ushauri kwa wanawake ambao wanapata maumivu makali wakati wa siku zao amewaomba kujenga tabia ya kwenda hospitali kuangalia afya zao kwani wengi wao hudhani maumivu ya tumbo kipindi cha siku zao ni tatizo la kawaida ambalo hukoma mara tu baada ya mtu kujifungua jambo ambalo sio kweli kidaktari.

Lakini pia amegundua tatizo alilonalo yeye ni wanawake wengi wamekumbwa na tatizo hilo hivyo ameshauri watu kwenda hospitali kwani uzazi limekuwa ni tatizo kubwa sana hapa nchini, na hii inaweza kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na mfumo wa maisha ambayo watu wanaishi pamoja na vyakula.

Pia ameshauri watu wasikae na vitu moyoni na kuwataka waseme ili wasaidiwe.

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Agosti 23, 2018
Mnangagwa alivyoishawishi Mahakama kutokubali ya Chamisa