Diwani wa kata ya Kawe CCM, Mutta Rwakatare leo ameingia kwa mara ya kwanza kwenye Baraza la Madiwani tangu kutokea kwa tukio la kupotea kwa muda mrefu na hatimae kukutwa maeneo ya Tabata akiwa kwa mwanamke mmoja ajulikanaye kama Ashura.

Mutta aliingia katika ukumbi huo wa kikao saa 7:22 mchana akiwa amevaa suti hali iliyowafanya madiwani wenzake waliokuwa ukumbuni hapo kumshangilia.

Mara baada ya kuingia diwani huyo alikwenda moja kwa moja kwenye viti walivyokaa madiwani na kusalimiana nao kwa kuwashika mikono na wengine kuwakumbatia na alivaa joho lake la Udiwani ambalo alilifuata eneo yalipowekwa mavazi hayo.

Akifungua kikao cha Baraza la Madiwani, Meya wa Manispa ya kinondoni Songoro Mnyonge, alitambua uwepo wa diwani huyo na kueleza kuwa wamefurahi kumuona tena.

“Tunashukuru mwenzetu Diwani Mutta aliyekuwa ametoweka na mimi kutangaza kwenye kikao kama hiki kuwa tunamtafuta lakini baadaye akarejea, tayari ametuahidi kuwa hatapotea tena karibu sana Mheshimiwa Mutta,” amesema Mnyonge huku akipigiwa makofi na madiwani kwa kugonga meza.

Meya Songoro amesema leo baada ya vikao na kazi wanatarajia kumfanyia sherehe ya kumkaribisha Diwani wa Kawe (CCM), Mutta Rwakatare ambaye alipotea mwanzoni mwa mwaka huu.

Diwani huyo ambaye ni mtoto wa marehemu Mchungaji Getrude Rwakatare, alipatikana Machi, eneo la Tabata akiwa nyumbani kwa mwanamke aliyejulikana kwa jina la Ashura na leo Ijumaa Juni 24,2022 alihudhuria kikao hicho jambo lililoamsha shangwe kutoka kwa wenzake.

IGP akemea vitendo vya mauaji
Geita Gold yafungiwa kusajili 2022/23