Diwani wa Kata ya Kiborlon, Manispaa ya Moshi, Frank Kagoma (Chadema), amefanya tukio la kishujaa kwa kupambana uso kwa uso na majambazi kadhaa waliokuwa wanamfyatulia risasi huku yeye akiwa mikono mitupu.

Akisimulia tukio hilo, diwani huyo alisema kuwa tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki majira ya saa tano asubuhi katika eneo la Kiborlon baada ya majambazi hao kuvamia duka moja la nguo za mitumba na kupora shilingi milioni 10 huku wakimjeruhi kwa risasi kichwani mmiliki wa duka hilo, Menti Mbowe. Majuruhi huyo anaendelea vizuri.

Diwani huyo alieleza kuwa alifika katika eneo hilo la tukio baada ya kupigiwa simu akielezwa uwepo wa majambazi hao, ndipo alipofika na gari lake huku akitoa taarifa kuomba msaada wa Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, alipofika kwenye tukio hilo anasema aliwakuta majambazi hao na kuonana nao uso kwa uso wakiwa na bunduki, huku wakitaka kummaliza lakini kwa ujasiri alipambana nao kwa kutumia gari lake.

“Nilipofika pale wale majambazi watatu ndiyo walikuwa wanatoka kwenye duka. Nikampelekea gari yule aliyekuwa ameshika bunduki. Kuona hivyo akafyatua risasi hewani,” anakaririwa na gazeti la Mwananchi.

“Yule mwenye bunduki akaingia uchochoroni kuelekea Barabara ya Stendi ya Kidia. Mwenzake aliyekuwa na bastola naye akawasha risasi nyingine hewani kunitisha,” alisimulia.

Alisema baada ya kuwakimbiza tena umbali fulani, walisimamisha pikipiki na kumfyatulia risasi nyingine mbili lakini alijificha kwenye kiti hivyo hakudhurika.

“Nililazimika kujificha kwenye kiti, wale majambazi wakajua wameniua. Wakapanda tena pikipiki ili watoroke. Nikawasha tena gari huku vijana wangu nao wakinisaidia tukaanza kuwafukuza,” alisema.

Kagoma alieleza kuwa baada ya kuwachanganya, walianza kukimbia na yeye akawafuata na gari lake huku akisaidiwa na vijana wa Bodaboda pamoja na Polisi ambao walikuwa wamewawekea mtego mbele ya barabara moja.

Alisema hata hivyo, majambazi hao waliingia katika barabara ambayo gari halikuweza kufika hivyo aliishia pale na kuwaacha vijana wa bodaboda wakiwafuatilia kabla ya kutokomea kwenye barabara yenye vumbi kali.

Akieleza sababu kuu ya kuwakosa majambazi hao, Kagoma alisema kuwa walikosea kutowapa taarifa polisi kwa kila njia waliyokuwa wanapita majambazi hao hali iliyowasababisha kukwepa mtego wa Polisi na kutokomea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa amesema kuwa atatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo leo mchana huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua wahalifu.

Per Mertesacker: Ushindani Utakua Mkubwa Msimu 2016/17
Video: 'Rais Magufuli Alikataa Kimemo Changu' - Makamba