Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Diwani wa Kata ya Bweri mjini Musoma, Dk Issack Chacha ameripotiwa kupigana ngumi kavukavu na Mwenyekiti wa Mtaa wa Songe, Hassan Mohamed wakidaiwa kumgombea Mtendaji wa Kata aliyetajwa kwa jina la Jamhuri Makongoro.

Tukio hilo limetokea katika ofisi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Songe wakati kikao alichoitisha kikiwa kinaendelea kabla ya kuingiliwa na Diwani aliyetaka kisitishwe ili aondoke na Ofisa Mtendaji huyo.

Kwa mujibu wa Mwananchi, Mweyekiti wa Mtaa wa Songe, Mohamed alikiri kutokea kwa tukio hilo akidai kuwa alijikuta akivaana kavukavu na Diwani huyo kwa sababu aliingilia kikao ambacho walikuwa wanajadili maendeleo ya mtaa wao.

Alisema kuwa Diwani huyo alimuita Ofisa Mtendaji huyo aliyekuwa ndani ya kikao hicho na kumtaka aondoke naye kwa madai kuwa alikuwa akimhitaji katika kikao chake kilichokuwa kikiendelea.

Naye Ofisa Mtendaji, Makongoro alikiri kushuhudia ugomvi huo wa ngumi kavukavu kati ya viongozi hao ambao wamedaiwa kuwa na msuguano wa muda mrefu.

Taarifa za ugomvi huo tayari zimemfikia Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Vicent Naano ambaye amesema ameanza kuzifanyia kazi.

Nahreel afichua siri ya 'Roma' kutoka Kimuziki, alichangia bila kumjua
Hillary Clinton Augua Ugonjwa wa Homa ya Mapafu, Donald Trump Achekekelea