Diwani wa Kata ya Ilala, Saady Khimji ametoa wito kwa Serikali na Mashirika binafsi kuisaidia Kampuni ya Dar Festival ili Iweze kufanya tamasha la kutangaza utamaduni wa nchi ya Tanzania.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Diwani huyo ambaye pia ni Mlezi wa Kampuni hiyo alipokuwa akilitangaza rasmi tamasha hilo mbele ya waandishi wa habari.

Khimji amesema kuwa ni jambo jema kuona vijana wanazungumzia suala la utamaduni kwani hali hii inaonyesha dhahiri kuwa wameamua kuirudisha nchi kwenye mstari wa kujali utamaduni wetu.

“Mataifa yote makubwa yanajali tamaduni zao hivyo ni vema na sisi kama watanzania kuamua kwa dhati kuhakikisha tunarudisha utamaduni wetu, jambo hili sio dogo linahitaji fedha nyingi kwahiyo, tunaomba msaada kutoka kwa Serikali na Mashirika binafsi ili kufanikisha tamasha hili”, alisema  Khimji.

Diwani huyo ameongeza kuwa vijana hao wamejitahidi hadi hapo walipofika lakini kama wakikosa misaada kutoka kwa wadhamini mbalimbali basi tamasha hilo halitoweza kufanikiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Faridi Faradji amesema kuwa  wameamua kuisaidia  Serikali  kwa kuangalia njia mbadala ya kukusanya mapato kwa kutangaza utamaduni wa Tanzania kupitia tamasha hilo.

“Kwa namna moja au nyingine,tuna kila sababu ya kuisaidia nchi yetu kukusanya mapato ili iweze kuendelea kwasababu baadhi ya nchi zingine zimeweza kuendelea kupitia matamasha kama haya”, alisema  Faradji.

Naye Katibu wa Kampuni hiyo, Amini Kingazi amesema kuwa tamasha hilo ni la asili kwahiyo wameamua kulifanyia katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa kwa sababu ni eneo lenye vitu vingi vinavyoonyesha utamaduni wa kitanzania.

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kila mwaka, Kwa mara ya kwanza litafanyika mwezi Septemba mwaka huu likijumuisha vitu vyenye asili ya kitanzania kama vyakula vya kitanzania, mashindano ya michezo ya kiasili pamoja na wanamuziki wa kitanzania

Waziri Mhagama Azindua Ripoti Ya Utafiti Wa Next Generation
24 Waitwa Taifa Stars