Polisi wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemkamata na kumfikisha mahakamani Diwani wa kata ya Kining’inila, Elisha Anthony (40) kujibu mashitaka mawili likiwemo la kutishia kumuua ofisa mtendaji wa kata hiyo, Fanty Haroun.

Mwendesha mashitaka wa Mahakama ya wilaya ya Igunga, Elimajid Kweyamba akimsomea mashitaka yake mbele ya hakimu Eddah Kahindi amedai kuwa Anthony anakabiliwa na mashitaka mawili ya kutishia kuua kwa maneno kinyume na kifungu 89 (2)(a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2002.

Shitaka la pili linalomkabili mshitakiwa huyo ni kutumia lugha ya matusi kinyume na kifungu cha 89 (1) (a) kanuni ya Adhabu sura ya 16 mapitio ya 2002.

Kweyamba ameeleza kuwa Januari 17, mwaka huu saa tisa alasiri katika kata ya kining’inila mkoani Tabora kwa nia ovu mshitakiwa alimtishia kumuua kwa maneno ofisa mtendaji wa kata hiyo.

Kwa upande wa Diwani ambaye ni mshitakiwa alikana mashitaka amabpo upande wa jamhuri ulidai upelelezi umekamilika.

Hata hivyo alipelekwa mahabusu hadi Februari 7 mwaka huu kutokana na kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana, ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja ambaye ni mtumishi wa Serikali na awe mkazi wa Igunga, awe na barua ya mwajiri wake na kitambulisho cha Taifa cha mpiga kura. pia atie saini dhamana ya Tsh. milioni tano.

TCRA kuwasaka waliosajiliana laini za simu
Video: JPM aibua mapya ya Kangi Lugola, Jaji mkuu ateswa utoaji haki kwa wakati