Katibu Mkuu Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Dk. Hassan Abbas amezitaka timu za ligi kuu na ligi za madaraja ya chini kuanza mazoezi, leo kwa kuwa Rais ameshatangaza ligi zinatakiwa kuanza Juni Mosi.

Rais John Magufuli alitangaza uamuzi huo jana jijini Dodoma baada ya kumuapisha Godwin Mollel kuwa naibu waziri wa afya kushika nafasi ya Dk Faustine Ndungulile ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. Pia aliapisha mabalozi na katibu tawala mmoja katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Dk. Abbas ambaye pia ni msemaji mkuu wa Serikali amesema timu zinapaswa kutumia muda uliosalia kufanya mazoezi ya pamoja, ili kurudisha umoja wao, kabla ya kuendelea kwa mshike mshike wa ligi kuu.

“Timu zinatakiwa kuanza mazoezi kuanzia leo kwakua Rais kashatangaza ligi inatakiwa kuanza Juni mosi kwahiyo ni ruhusa kufanya mazoezi,” amesema Dk. Hassan Abbas, Katibu Mkuu Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo.

Hata hivyo Bodi ya ligi pamoja na TFF bado hawajatoa tamko rasmi kuhusu muda wa kufanya mazoezi utakaotolewa kwa vilabu vya ligi kuu na ligi za madaraja ya chini, kabla ya kuendelea kwa michuano ya soka nchini.

Ligi Kuu ilisimamishwa Mach 17, siku moja baada ya Serikali ya Tanzania kutangaza mtu wa kwanza kugundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo ulioua zaidi ya watu 320,000 kote duniani na kuambukiza zaidi ya watu milioni 4.1.

Ligi kuu ilisimamishwa wakati mabingwa watetezi Simba wakiongoza kwa zaidi ya pointi 17 juu ya Azam inayoshika nafasi ya pili, huku Young Africans ikiwa pointi moja chini.

Burundi watakiwa kuwa watulivu, matokeo wiki ijayo
Waziri Kairuki avutiwa na uwekezaji kiwanda cha mafuta ya alizeti