Agizo la Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuzuia waliofeli kidato cha nne na baadae kujiendeleza ngazi ya cheti na stashahada wasiruhusiwe kujiunga vyuo vikuu kuchukua shahada, umepingwa vikali na wasomi akiwemo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana.

Mhadhiri huyo amesema kuwa uamuzi huo wa Profesa Ndalichako sio sahihi na kwamba ni kinyume cha utaratibu wa elimu kote duniani.

“Kama amechukua uamuzi huo nafikiri amekurupuka, kama anafikiria kidato cha sita ndiyo njia pekee, ameshauriwa vibaya na huo uamuzi aufute haraka sana na ni kinyume na utaratibu wa elimu kote duniani,” Dk. Bana anakaririwa na Mtanzania.

“Utakuwa uamuzi wa dhambi ya asili na dhambi ya ubaguzi. Kama anataka njia ya kuboresha elimu aje tumfundishe,” aliongeza.

Alisema kuwa yeye pia ni mmoja kati ya wasomi ambao hawakusoma masomo ya kidato cha tano na sita na hadi sasa wana nafasi kubwa katika ulimwengu wa taaluma na wanaheshimika duniani.

Aliwataja wasomi wengine ambao hawakupitia kidato cha tano na sita kuwa ni pamoja na Profesa Mwesiga Baregu ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT). Mwingine ni aliyekuwa Makamu Mkuu wa UDSM kwa kipindi cha miaka 14, Profesa Methew Luhanga.

Naye Profesa Baregu alionesha kushangazwa na agizo hilo la Profesa Ndalichako na kudai kuwa hafahamu sababu iliyopelekea kutoa uamuzi huo badala ya kujenga mazingira bora ya watu kujiendeleza kielimu. “Sijamuelewa waziri, kwanini ameona diploma kwenda chuo kikuu ndiyo tatizo,” alisema msomi huyo.

Berlusconi: AC Milan Tayari Imeshauzwa
Chadema waja na oparesheni ‘Kata Funua’