Naibu waziri wa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla ameweka mtego na kuwanasa watumishi wa ofisi za wizara hiyo wanaochelewa kufika kazini.

Jana waziri huyo aliwahi katika ofisi za wizara hiyo akiwa anatembea kwa miguu (huenda alipaki gari lake nje kwa mbali) na kuingia ofisini kwake.

Ilipotimia majira ya saa moja na nusu asubuhi ambao ndio muda wa mwisho wa wafanyakazi kuingia ofisini, Dk. Kigwangalla alielekea katika geti la ofisi hiyo na kuwataka walinzi kufunga geti ili abaini waliochelewa kufika ofisini.

Kadhalika, Naibu waziri huyo alimuagiza Mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu kupiga mstari wa kufunga kwenye daftari la mahudhurio la wafanyakazi wizarani hapo ili aweze kubaini wafanyakazi ambao wamechelewa.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Dk. Kigwangalla alieleza kuwa ameamua kufanya hivyo ili kubaini wachelewaji na nia ya watumishi hao kufanya kazi kwa kasi anayoitaka rais John Magufuli.

“Nina wiki moja tangu nimeingia hapa ofisini, kuna mambo ambayo nimeyaona hayapo vizuri na sasa naanza na hili ili tujue kuwa  ni kina nani huwa wanachelewa na zoezi hili litakuwa ni endelevu, kama mimi sitasimamia watumishi wa serikali basi sitakuwa na kazi, wizarani tunataka watumishi ambao wanakuwa wanafanya kazi kwa kujitoa kwa ajili ya maslahi ya taifa.”

Dk. Kigwangalla aliagiza watumishi wote waliochelewa kuandika barua za kujieleza huku akimuagiza Mkurugenzi Mkuu kuhakikisha anafanya marekebisho na kuweka mfumo wa ‘Bio-metric’ wa kutumia kadi au kidole kujiorodhesha kwa mtumishi anapoingia kazini badala ya kutumia daftari.

CAG Adaiwa 'Kuibipu' Nyundo ya Magufuli, Akiuka Agizo Lake
Ukosefu wa Madarasa wazuia Wanafunzi 12,225 kuingia kidato cha Kwanza Dar