Wakati vuguvugu la kuzijibu hoja za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbroad Slaa zikiendelea, ameibuka tena na kutoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wake wa kumvaa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.

Akiongea Tido Mhando wa Azam TV, Dk Slaa alieleza sababu za kumshambulia Edward Lowassa pekee kwa hoja za ufisadi huku akiiacha CCM ambayo siku zote amekuwa akiituhumu kukumbatia ufisadi.

Alisema amechukua uamuzi huo kwa kuwa haoni sababu za kumuongelea mtu mwingine kwa kuwa Lowassa atakuwa rais wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano.

“Tido nilielezea mfumo juu ya serikali ya CCM akiwemo Rais Kikwete kuwa ndiyo waliomlea Lowassa. John Mnyika aliwahi kusema Bungeni kuwa Kikwete ni dhaifu hilo halina utata, lakini hivi sasa hatumzungumzii Kikwete kwa kuwa ameshaondoka na ameshaagwa,” alisema.

“Tunapoteza muda kwa mtu ambaye kesho hayupo, hapa tunamzungumzia mtu ambaye tutakuwa naye kama rais wetu kwa miaka mitano ijayo,” aliongeza.

Aliongeza kuwa anamzungumzia Lowassa kwa kuwa madhara yake ni makubwa kuliko watu wengine.

D.k Slaa amekuwa akikosolewa na wafuasi wa Ukawa kwa madai ya kumshambulia mgombea mmoja tu wa urais (Edward Lowassa) bila kumgusa mgombea wa CCM, Dk John Magufuli ambaye chama chake kinatajwa kuwa na mfumo unaokumbatia ufisadi.

Wafuasi hao pia walimtuhumu kuwa amenunuliwa na CCM ili awasaidie kumsema Lowassa kwa lengo la kuhujumu kampeni za mgombea huyo.

Hata hivyo, Dk Slaa ambaye alitangaza kustaafu siasa za vyama, alidai kuwa ukweli hauwezi kuwa na pande mbili hivyo ukweli wake lazima uegemee upande mmoja.

Katibu huyo wa zamani wa Chadema alizungumza hayo masaa machache kabla ya Askofu wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kujitokeza kujibu tuhuma zake.

 

 

Chadema Yaruka Viunzi Tuhuma Za Udini Dhidi Ya Lowassa
Bomu La Gwajima Limempata Dk. Slaa?