Ugomvi wa maneno kati ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema limemuibua katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa aliyeandika ujumbe mrefu akimkingia kifua mbunge huyo.

Gambo na Lema walirushiana maneno juzi mbele ya wafadhili kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maendeleo wa ujenzi wa hospitali itakayohudumia bure wanawake na watoto uliogharimu shilingi bilioni 9.

Kupitia ujumbe huo uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambao alithibitisha kuwa ni wa kwake, Dk Slaa amemrushia lawama Mkuu huyo wa Mkoa akidai kuwa anaijua vizuri historia ya ardhi na mradi huo.

“Mrisho Gambo, busara na hekima ya kawaida ingelikuwezesha kuelewa barua ya mwaliko ambayo imesisitiza mara mbili hivi kuwa wahusika ni taasisi isiyojulikana na siasa,” imeeleza sehemu ya ujumbe wa Dk Slaa.

Aliongeza kuwa endapo mkuu huyo wa mkoa angetenganisha siasa na mradi huo wa maendeleo kama alivyoshauriwa na kwenye barua yake ya mwaliko wasingefikia katika hatua hiyo iliyolitia taifa aibu.

Dk Slaa ambaye aliitosa Chadema na kutangaza kustaafu siasa na hivi sasa anaishi nchini Canada, amesema kuwa anazitambua juhudi za Lema kuwa ndio chimbuko la upatikanaji wa ardhi hiyo.

“Historia haifutwi kwa propaganda jukwaani. Lakini kwa bahati mbaya athari za propaganda imeenda mpaka kuchafua Taifa letu kwa wahisani,” ameandika.

Akieleza kwa ufupi anachokifahamu kuhusu ardhi hiyo, alisema kuwa Lema ndiye aliyepata ardhi hiyo kutoka kwa familia ya Wakili Mawala ambaye hivi sasa ni marehemu.

Dk Slaa alifanya mahojiano kwa njia ya simu na Mtanzania na kuthibitisha kuwa ujumbe huo ni wake.

Wachina Kumrudisha Big Sam Stadium Of Light
Wekundu Wa Msimbazi Simba Wasisitiza Ushindi