Aliyekuwa Katibu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa ametoa majibu ya baadhi ya maswali yanayoulizwa na wananchi baada ya hotuba yake iliyomshambulia kwa tuhuma za ufisadi Edward Lowassa na chama hicho.

Akiongea katika mazungumzo maalum na Azam TV, Dk Slaa ameelezea kuhusu suala la alikotoa fedha za kugharamia matangazo ya televisheni na ukumbi wa hotel ya kitalii ya ‘Serena’.

Dk. Slaa amekiri kuwa tukio hilo liligharamiwa na watu wengine japo hakuwataja watu hao, na kudai kuwa hiyo sio mara ya kwanza watu wengine kumgharamia.

“Kwanza nawashangaa, hivi mwaka juzi, mwaka jana nimeenda Marekani sikuulizwa hizo gharama,” alisema na kudai kuwa Chadema hawakuwahi kugharamia ziara yake nchini Marekani na kuwataka watoe vielelezo kama waliwahi kufanya hivyo.

“Waweke hadharani senti hata moja ya chama kulipia safari ya Dk. Slaa Marekani,” alisema. Hata hivyo alibainisha kuwa chama hicho kilimlipia shilingi laki tano kwa ajili ya kuandaa nyaraka alizoendanazo Marekani.

Katika hatua nyingine, Dk Slaa ambaye alitangaza kustaafu siasa, alikanusha habari zilizoenea kuwa amekimbia nchi kuelekea nchini Canada, mara baada ya kutoa hotuba yake.

“Wanasema sipo tena Tanzania, nilishaondoka toka tarehe ile nilipomaliza press conference tu, lakini mimi niko hapa na wewe tuko Azam studio, kwa hiyo unaweza ukaona aina ya upotoshwaji uliokuwepo,” alibainisha.

Dk. Slaa anadaiwa kutumiwa na Chama Cha Mapinduzi kudhoofisha kampeni za urais za Ukawa na kwamba chama hicho tawala kilimuandalia mkutano huo na waandishi wa habari pamoja na gharama za kurusha matangazo ya Televisheni zinazokariwa kuwa zaidi ya milioni 89.

Madai yanayotolewa na baadhi ya uongozi wa Ukawa yalieleza kuwa Dk Slaa anachuki na hasira ya kunyimwa nafasi ya kugombea urais kupitia umoja huo, nafasi aliyopewa Edward Lowassa aliyepokelewa na Chadema akitokea CCM.

 

 

Van Gaal Akubali Yaishe, Amjumuisha Valdes Kikosini
JK amshangaa Tena Sumaye