Baada ya ukimya wa muda mrefu kuhusu kile kinachoendelea ndani ya Chadema na taarifa za kukiacha chama hicho, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa ametoa taarifa ya kusikitisha kuwa maisha yake na familia yake yako hatarini.

Dk. Slaa ameweka wazi hofu yake jana alipokuwa akifanya mahojiano na mwandishi wa Raia Tanzania kwa madai kuwa ameona aiweke hadharani hali hiyo ili chochote kitakachotokea watanzania wafahamu.

“Ni dhahiri ninatengenezewa mizengwe ya kila aina. Inaonekana maisha yangu na ya familia yangu sasa yako hatarini. Nimekuambia (mwandishi) ili ikitokea chochote ujue siyo bahati mbaya. Sijawahi kuogopa na wala sitaogopa. Mtetezi wangu ni Mungu aliyehai na nina hakika atanilinda kama yanayopangwa sio mapenzi yake. Kama ni mapenzi yake yatimie na isiwe kama ninavyotaka mimi,” Dk. Slaa amekaririwa na gazeti la Raia Tanzania.

Kufuatia kuwepo taarifa zisizo rasmi kuwa Dk. Slaa amejitoa Chadema na ana mpango wa kuacha kabisa siasa akipinga uamuzi wa chama hicho kumkaribisha Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea urais, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe jana alisema kuwa atazungumzia saula hilo muda utakapofika.

Taarifa zilizopatikana kutoka katika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kinachoendelea, suala la Dk. Slaa ni moja kati ya mijadala itakayowekwa mezani. Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Dk. Slaa atajadiliwa kwa kuwa yeye ndiye alitoa wazo la kumpokea Edward Lowassa hata kabla hajakatwa kwenye mchakato wa kura za maoni CCM.

“Suala la Dk. Lazima na lenyewe lijadiliwe kwa sababu yeye ndiye aliyeleta wazo la kumpokea Lowassa kabla hata hajatoka CCM. Mwanzoni kabisa kwenye kikao cha siri, Dk. Alisema kuna kila dalili ya Lowassa kukatwa na chama chake hivyo akashawishi kwamba ni vyema Chadema imchukue,” Chanzo kutoka Chadema kilikaririwa na gazeti la Mtanzania.

 

 

Di Maria Atua Mjini Doha, Qatar
Ole Sendeka Azungumzia Taarifa Za Kuhamia Chadema