Wingu jeusi lililokuwa limetanda juu ya wanachama wa Chadema kuhusu hatma ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa limeanza kufifia baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuweka wazi kinachoendelea.

Akizungumza na wanachama katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Mbowe alieleza kuwa wamekubalina na Dk. Slaa apumzike kwa muda baada ya kushindwa kubadili msimamo wake wa kutokubaliana na uamuzi wa chama hicho kumkaribisha Edward Lowassa.

Mbowe ameeleza kuwa awali viongozi wa ngazi za juu za chama hicho zilifanya vikao kadhaa kujadili uamuzi wa kumkaribisha au kutomkaribisha Lowassa na kwamba kulikuwa na mvutano mkubwa wa mawazo lakini mwishoni wote walikubaliana kuwa huo utakuwa uamuzi wa chama.

“Tulifanya majadiliano ambayo yaliambatana na kazi ya kitakwimu na ya kisayansi kiutafiti tukaridhika pasipo shaka kwamba ugeni wa mheshimiwa Lowassa na wenzake katika chama chake ni mpango wa Mungu,” alisema Mbowe.

“Katika hatua zote hizo, tulikuwa sambamba na mheshimiwa Dk. Wilbroad Slaa. Katika dakika za mwisho, Dk. Slaa akatofautiana kidogo na Kamati Kuu. Tukajaribu kuzumza nae kwa kina sana, hata jana nilikuwa na kikao cha kina na Dk. Slaa kwa masaa mawili, tulikuwa na kikao nae jana mchana.

“Kwa hiyo tukakubalina kimsingi na Slaa kwamba sisi tuendelee. Katika hatua atakapokuwa tayari atatujoin mbele ya safari tutakuwa na Dk. Slaa pamoja. Kwahiyo, tumemkubalia Dk. Slaa mapumziko ili tuendelee kuliandaa taifa hili kwa ajili ya uchaguzi,” alisema.

Mbowe alisisitiza kuwa hakuna ugomvi wa ziada kati yao na Katibu Mkuu huyo nakuwataka wanachama kutosikiliza uzushi unaoripotiwa kwenye mitandao ya kijamii.

My Take: Kama ambavyo Chadema wanaiombea CCM njaa ili washindwe vita ya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba, ndivyo ambavyo CCM inawaombea.

Taarifa za kuwepo mtafaruku na kutoelewana kati ya viongozi wa Chadema na Dk. Slaa ambaye anaushawishi mkubwa ni mtego mzuri ambao CCM wanausubiri unase ili wapate jinsi ya kukishambulia chama hicho kwa hoja wakidai kuwa mgombea waliyempokea hasafishiki hata kwa Dk. Slaa aliyemtaja kuwa fisadi kwa kipindi cha miaka 8.

Hata hivyo, bado haifahamiki kama Dk. Slaa atakuwa mapumzikoni kwa muda gani huku ikifahamika kuwa lazima atashawishiwa na wapinzani wa Chadema akimwage chama hicho. Je, nini kitatokea katika mapumziko hayo yasiyojulikana? Je, akimaliza mapumziko atarudi Chadema yenye Lowassa ama ataamua vinginevyo?

 

Nuh Mziwanda Na Shilole Wazungumzia Sauti Ya Nuh ‘Akimtongoza’ Wema Sepetu
Dk. Slaa Kuiokoa Chadema Dhidi Ya Mtego Wa CCM?