Msemaji wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amewataka Watanzania kutembea kifua mbele kwani Tanzania imeongoza kwa kasi ya kupunguza umasikini Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 3, 2019 jijini Dar es Salaam, Dkt. Abbasi amekariri ripoti mbili za taasisi za kimataifa ikiwa ni pamoja na Ripoti ya Benki ya Dunia na ya ‘Human Capital’, zinazoonesha kuwa Tanzania imeongoza kwa kasi ya kupunguza umasikini katika ukanda huo.

“Ripoti ya Septemba 6, 2019 ya Benki ya Dunia imeeleza kuwa Tanzania imeongoza kwa kupunguza umaskini miongoni mwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara,” amesema Dkt. Abbasi.

“Julai, 2019 ripoti nyingine ya WB “Human Capital; The Real Wealth of Nations” imeonesha umaskini nchini umepungua kutoka 34.4% hadi 26.8%,” ameongeza.

Aidha, Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli imefanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo kwani zaidi ya miradi 289 na vituo zaidi ya 89,780 vilivyotumia Sh. 336.15 bilioni vimekamilika.

Ameongeza kuwa kazi kubwa inaendelea kufanyika na kwamba hadi sasa vituo 44,590 vya maji katika maeneo ya vijijini vinaendelea kukamilishwa.

“Hadi Septemba mwaka huu zaidi ya miradi mikubwa 17 ya maji imekamilika ambapo zimetumika zaidi ya Sh 823.61 Bilioni. Wakati miradi mingine mikubwa zaidi ya 35 ya maji ikiendelea kukamilishwa nchini,” Dkt. Abbasi amesema.

Ameeleza kuwa hali ya upatikanaji wa maji mijini imeendelea kuimarika, hadi sasa upatikanaji wa maji safi mijini umefikia asilimia 80.

Katika hatua nyingine, Msemaji huyo wa Serikali ameeleza hatua ambayo Serikali imefikia katika kuwakomboa wakulima wa Korosho. Ameeleza kuwa Serikali imenunua korosho kwa bei ya kati ya Sh 330,000 hadi 1,500 inayomfaidisha mkulima ikitumia Sh 720 bilioni.

“Niwahakikishie wakulima kuwa hadi kufikia Septemba 30, 2019, Serikali imeshauza korosho zote kwa jumla ya wanunuzi 21 wa ndani na nje ya nchi. Kuna tani zaidi ya 4,595.90 zitabanguliwa nchini na zaidi ya tani 211, 587 ambapo tani 107,187 zitapitia Bandari ya Dar es Salaam na tani 104,400 kupitia Bandari ya Mtwara zitasafirishwa kwenda nje ya Tanzania,” amesema.

Ameongeza kuwa hadi sasa zaidi ya tani 98,860 zimekwishachukuliwa na kusafirishwa nje ya nchi kupitia Bandari za Mtwara na Dar es Salaam, ikiwa ni sawa na 41% ya korosho zote; na kwamba zoezi la kuondoa korosho iliyobaki kupelekwa kwa wanunuzi linatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 21 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali, zoezi hilo limewasaidia wakulima kupata bei ya haki na kwamba limesaidia kuweka mazingira bora zaidi na mfumo madhubuti ya kulinda haki za wakulima na kuimarisha kilimo cha zao hilo.

Kadhalika, Dkt. Abbasi ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imevunja rekodi baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi ya Sh 1.7 trilioni kwa mwezi, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tangu  nchi ilipopata uhuru kutoka kwa wakoloni.

Yanga, Polisi Tanzania hakuna mbabe
Jafo awataka Wakurugenzi wapya kusimamia majukumu yao kikamilifu