Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amezungumzia kasi ya ukuaji wa Chama cha ACT-Wazalendo na ushindani itakaouleta kwa chama hicho tawala.

Akizungumza wiki hii na ZBC2, Dkt Bashiru amesema kuwa wanafurahi kuona chama cha siasa kinazidi kuimarika kuliko kuharibika kwani wanahitaji kuwa na washindani madhubuti.

Alisema kuwa ACT-Wazalendo haiwezi kuwa tishio kwa CCM kwani bado ina safari ya kujiimarisha kwa kuzingatia kuwa ina muwakilishi mmoja pekee ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo huenda wakapata nafasi ya kuongeza idadi ya wawakilishi tu.

Akizungumzia mpasuko wa Chama Cha Wananchi (CUF) uliosababisha baadhi ya viongozi wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad kujiunga na ACT-Wazalendo kwa kutumia msemo “shusha tanga, pandisha tanga”, Dkt Bashiru alisema haikuwa na shida kama tu haiathiri amani na umoja wa Watanzania.

“lle shusha tanga pandisha tanga haikuwa na shida ila tu isivunje umoja wala amani. Hata sisi tulishtuka hatukutarajia mabadiliko yale kwa sababu hatukujua chama kama kile kinaweza kuwa na mgogoro wa ndani na kusababisha mpasuko, lakini tunashukuru Mungu mambo yameenda salama,” alisema Dkt. Bashiru.

Ametoa rai kwa vyama vya siasa kuendeleza ushindani madhubuti bila kuathiri amani na umoja uliopo kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.

Wabunge Uganda wajiongezea mshahara
“Pogba hataki kuwa Manchester United”