Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amekabidhi Mbuzi mnyama na kilo 20 za mchele kwa kituo cha Watoto Yatima cha Rahim kilichopo Igelegele, wilayani Nyamagana na kuwashauri watu wanaotaka kuanzisha vituo vya kulea watoto yatima wawe na mipango ya miradi endelevu.
 
Hayo yamesemwa na Katibu wa CCM mkoani Mwanza, Salum Kalli wakati akikabidhi zawadi hiyo kwenye kituo hicho kwa niaba ya Dkt. Bashiru Ally ambapo amewataka watakaoanzisha vituo vya kulea watoto yatima wawe na mipango na wafikirie kubuni na kuanzisha miradi endelevu itakayowasaidia watoto.
 
“Tuhakikishe tunakuwa na miradi ama tubuni miradi endelevu badala ya kuwa ombaomba kwani ipo siku wafadhili wakigoma hali itakuwa mbaya kwa watoto hawa yatima japo dini inatutaka tuwahudumie wajane na yatima na kama hatuna uwezo, tusilazimishe wakati hatuwezi kuwatimizia mahitaji yao ya elimu, matibabu, malazi na chakula,”amesema Kalli.
 
Katibu huyo wa CCM amewaasa watoto hao zaidi ya 70 kujituma na kujibidiisha katika masomo yao ya elimu ya dini na mazingira kwani urithi pekee wanaohitaji ni elimu iweze kuwasaidia kwenye maisha yao siku za usoni.
 
“Dkt. Bashiru kaonyesha upendo kwenu na kanituma niwaletee zawadi hii ya kitoweo na mchele. hivyo mjifunze kwa makini, upendo, mthaminiane, muelekezane kwa mema na kukataa mabaya ili wengine huko nje wajifunze kutoka kwenu, pia sisi viongozi ujio wetu tutajifunza mengi kutoka kwenu na yawezekana ujio huu ukafungua kheri,”amesisitiza Kalli.
 
Kwa mujibu wa Kalli, Dkt. Bashiru, akiwa kwenye ziara yake wilayani Magu, wananchi wa Kijji cha Ndagalu walimzawadia Mbuzi na yeye akaamua kumtoa Mbuzi huyo na kilo 20 za mchele katika kituo hicho cha yatima.

RC-Moro azungumza baada ya majeruhi mwingine ajali ya lori kufariki dunia
Wafanyakazi wa NMB wazama baharini Tanga