Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amewaonya wakuu wa mikoa ya Morogoro, Dkt. Steven Kebwe na mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella juu ya kutosimamia ipasavyo shughuli za serikali katika maeneo yao.

Ametoa onyo hilo jana wakati akitoa salamu za chama cha mapinduzi katika maadhimisho ya kilele cha maonyesho ya wakulima (Nanenane) yaliyofanyika katika viwanja vya Nyakabindi, wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

Amesema kuwa Dkt. Kebwe ameshindwa kumshughulikia mkurugenzi wa halmashauri iliyo chini yake ambaye anadaiwa kutumia shil. milioni 60 zilizotolewa kwaajili ya matumizi maalum kununua dawa ya mchwa.

Aidha, Dkt. Bashiru amesema kuwa kitendo hicho kilichomshinda mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe mpaka pale Rais Magufuli alipoamua kumtumbua mtu huyo, hivyo ni tafsiri kwamba mtu huyo ameshindwa kusimamia majukumu yake.

Pia Dkt. Bashiru amemuonya mkuu wa mkoa wa Mwanza, RC Mongella huku akimtaka kumsimamia na kumbana mkurugenzi wa Halmashauri ya Sengerema aliyeshindwa kutaja kiwango cha bajeti ya miundombinu ya barabara.

”Nisitoke hapa bila kumlaumu mmojawapo katika timu iliyopo serikalini kwa nia njema kabisa ili mwaka kesho naye ajirekebishe nadhani mkuu wa mkoa wa Morogoro na mkuu wa mkoa wa Mwanza ujumbe wangu mmeupata, haya yote ni kwaajili ya kujenga, timizeni majukumu yenu,”amesema Dkt. Bashiru

Hata hivyo, Dkt. Bashiru amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na mawaziri wake kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya chama hicho tawala katika maeneo ya Simiyu na Mwanza.

Video: Dkt. Bashiru Ally amtaka Waziri Mkuu kusimamia watendaji
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 9, 2019