Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amewataka wajumbe wa mashina (mabalozi) kutopanga foleni kwenye ofisi yoyote iwe ya CCM au ya Serikali.

Ameyasema hayo wilayani Magu mkoani Mwanza alipokutana na wanachama, mabalozi, na wajumbe wa halmashauri kuu kata zote na matawi yote wilayani humo katika vikao vitatu tofauti.

Amesema kuwa, mabalozi nchi nzima hawatakiwi kukaa foleni katika ofisi yoyote ya serikali na chama, kuanzia ofisi za watendaji wa mitaa, watendaji wa kata, wakuu wilaya, wakurugenzi, wakuu wa mikoa mpaka ofisi za wizara yoyote nchini, kwa sababu mabalozi ndio watu wanaofanya kazi kuliko kiongozi yeyote, kwa kuhangaika na changamoto za mwananchi mmoja mmoja katika eneo lake, bila ya mshahara.

“Nitoe rai kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi nchi nzima kwa viongozi wa serikali na Chama, wakuu wilaya na mikoa, wakurugenzi wote wa Halmashauri nchi nzima, makatibu wa wilaya na mikoa nchi nzima, hawa viongozi wetu wajumbe wa mashina ni marufuku kukaa foleni kwenye ofisi zenu, hawa ni viongozi na wamebeba watu nyuma yao, wanapokuja ofisini wanakuja kueleza hisia, changamoto, na ushauri wa watu wao wanaowaongoza. Kiongozi yeyote atakaye wadharau mabalozi wetu huyo hatufai ndani ya Chama na serikali hii ya CCM.” amesema Dkt. Bashiru

Aidha, Dkt. Bashiru amekazia maelekezo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwataka viongozi wote kuanzia ngazi za msingi mpaka taifa kutenga muda katika maeneo yao kuwa karibu na wananchi, kuwasikiliza kero zao, na kuwapatia ufafanuazi.

Akiwa wilayani Magu Katibu Mkuu ameweka jiwe la msingi na kushiriki ujenzi wa hosteli za CCM na kukagua mradi wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) wa ufugaji wa Ng’ombe wa maziwa ambapo amewaongezea Ng’ombe mmoja ili kuimarisha mradi utakaowezeshe shughuli za Chama na Jumuiya.

Waajiri nchini watakiwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu
Mtangazaji wa DW afariki Dunia