Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amewaonya wanachama wa chama hicho ambao wanatumia mitandao ya kijamii kufanya fitna na hujuma.

Dkt. Bashiru ametoa onyo hilo leo alipokuwa akihitimisha ziara yake mkoani Geita, ambapo amewataka wanaofanya vitendo hivyo kupitia mitandao ya kijamii kuwajibishwa na vikao husika.

“Watu wengi wanapoteza muda kwenye mitandao na sana sana wanayovizungumza ni porojo si mambo ya kujenga, tumekubaliana mwananchama yeyote atakayetumia vibaya mitandao kumhujumu mwenzake, kufitini na kuzua mambo ambayo yanaleta mtafarufu ndani ya chama, vikao vya chama vichukue hatua haraka inavyowezekana,” amesema Dkt. Bashiru.

Aidha, kiongozi huyo ametahadharisha kuwa, CCM haitatumia fedha za matajiri kufadhili shughuli zake za kichama bali itatumia miradi ya chama na michango ya wananchama wake.

Ili kufanikisha hilo, amesisitiza kuwa michango ya wanachama ikusanywe kwa ufanisi pamoja na kuwahamasisha wanachama kutoa michango ya hiari ya kuwezesha shughuli za chama hicho tawala.

Tangu alipoteuliwa, Dkt. Bashiru amekuwa akisisitiza kuhakikisha chama hicho hakitumiwi na watu waliokuwa wanatajwa kuwa na jeuri ya fedha au nguvu ya kifedha ili haki ya kila mwanachama ilindwe.

Morali ya kufanya kazi ya Kibunge imepungua- Godbless Lema
‘Marufuku daladala kuingia katikati ya jiji, watu wafanye mazoezi’