Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amebariki mjadala kuhusu Katiba Mpya ulioibuka Bungeni na kuzua vita ya hoja kwa hoja kati ya wabunge wa chama hicho na wale wa Kambi ya Upinzani.

Dkt. Bashiru amesema kuwa mjadala huo ni mzuri na ni afya kwa ustawi wa demokrasia nchini kwani wabunge wamejadili hoja bila kutukanana.

“Ninafuatilia mjadala unaoendelea Bungeni na wanavyojadili kuhusu Katiba Mpya, hoja kwa hoja, malumbano bila kutukanana ndiyo afya ya demokrasia. Nachelea kuzungumzia suala hili kwa sababu nitaufunga mjadala,” amesema Dkt. Bashiru alipohojiwa na gazeti moja.

Mjadala huo ulianzishwa na Mbunge wa Viti maalum wa Chadema, Salome Makamba wakati wa kupitisha Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020. Mbunge huyo  alidai kuwa katika ukurasa wa 106, 107 wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 imeahidi kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.

“Dkt. Bashiru anapita sehemu mbalimbali anasema wanatekeleza ilani ya CCM, ni kama mnawalaghai wananchi na mnasema tunaishi katika Katiba, ni Katiba gani hiyo?” Alihoji mbunge wa Chadema, Susan Lyimo akichangia katika mjadala huo.

Hata hivyo, wabunge wa CCM walijibu hoja hiyo na kuendelea kuhuisha majibizano ya hoja baada ya kueleza kuwa wabunge wa upinzani ndio waliokataa kuendeleza mchakato wa Katiba kwa kutoka nje ya Bunge la Katiba.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi alijibu hoja zilizotolewa akieleza kuwa Katiba ni dira na mwongozo wa nchi na kwamba mchakato wa kupata Katiba mpya utaendelea kwa kuzingatia mahitaji na mazingira yanavyoruhusu.

 

Mrithi wa Nassari ameahidi makubwa Arumeru
TANAPA yachangia ujenzi wa Zahanati mkoani Kagera