Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusitisha uagizaji wa viunganishi vya miundombinu ya umeme (Accessories) kutoka nje ya nchi badala yake wanunue hapa hapa nchini.

Ametoa agizo hilo alipotembelea Kiwanda cha uzalishaji viunganishi cha Auto Mech Ltd kilichopo Tabata jijini Dar es Salaam ili kujionea uwezo wa Kiwanda hicho katika uzalishaji viunganishi hivyo.

“Nimekuja hapa ili kujiridhisha kama Kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha viunganishi vya kutosha, nimejiridhisha kuwa, kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha viunganishi hivyo, kwa hiyo nimetoa miezi mitatu ili TANESCO, REA na Wakandarasi wote kwa pamoja wajiandae sasa kununua vifaa hivi nchini.” Amesema Dkt. Kalemani

Aidha, amesema kuwa miezi mitatu iliyopita alisitisha uagizaji wa Mita za luku na nguzo kutoka nje lakini baado kuna changamoto ya wananchi kuchelewa kuunganishiwa umeme na tatizo kubwa ni ukosefu wa viunganishi hivyo.

Hata hivyo, Kalemani ameogeza kuwa manufaa ya kutembelea kiwanda hicho ni kujiridhisha kuwa kina uwezo mkubwa wa kuzalisha viunganishi hivyo na hatimae kuokoa gharama kubwa ya uagizaji viunganishi hivyo kutoka nje ya nchi.

 

Vyakula 5 vinavyopunguza hatari ya maambukizi ya kansa mwilini
Wachezaji wa kombe la dunia kucheza dhidi ya Leicester City