Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema Serikali imeweka mfumo mzuri katika usimamizi wa Sekta ya Madini ili kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini vinavyofanywa na baadhi ya wachimbaji pamoja na wafanyabiashara wasio waaminifu hapa nchini.

Akiongea katika Mgodi wa Irasanilo Gold Mine, uliopo kijiji cha Magunga Kata ya Buhemba Wilaya ya Butiama Mkoani Mara Desemba 4, 2022, Dkt. Kiruswa amesema Serikali ipo makini na imeweka mifumo imara ya kudhibiti na kuwabaini wote wanaojishughulisha na utoroshaji wa madini katika maeneo mbalimbali.

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa anasema Serikali imeweka mfumo mzuri katika usimamizi wa Sekta ya Madini ili kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini vinavyofanywa na baadhi ya wachimbaji pamoja na wafanyabiashara wasio waaminifu hapa nchini.

Amesema, “Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo macho, Serikali ipo kazini usiku na mchana na watu wanaojaribu kutorosha madini ni kama wamejichukia wanataka kuharibu maisha yao.”

Akizungumza malalamiko yaliowasilishwa na wachimbaji wadogo katika mgodi huo, juu ya kutozwa tozo ya Halmashauri ya shilingi 1000 kwa kila mfuko wa mawe Dkt. Kiruswa amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Butiama kukaa kikao na viongozi wa mgodi huo ili kujadili kwa pamoja suala hilo.

Sehemu ya Wananchi wa Kijiji cha Magunga Kata ya Buhemba Wilaya ya Butiama Mkoani Mara, waliokuwa wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa (hayupo pichani)

Aidha, amewataka wachimbaji wadogo kuchoma dhahabu ya Zebaki katika eneo moja lililotengwa na Serikali na kutumia teknolojia ya Kigida katika uchomaji ili kudhibiti uzalishaji wa madini pamoja na kutunza afya, usalama wa wachimbaji na utunzaji wa mazingira.

Kwa upande mwingine, Dkt. Kiruswa ameweka jiwe la msingi katika jengo jipya la Soko la Madini Irasanilo ambalo linajengwa na mgodi huo ili kurahisisha uuzaji wa madini ya dhahabu na kusisitiza ujenzi ukamilishwe haraka ili kusaidia wachimbaji katika eneo hilo na kuwepo na maafisa wa Serikali kwa ajili ya kutoa huduma kwa wachimbaji.

Wafanyakazi wa mgodini wakiwa katika majukumu ya kila siku.

Naye, Mkuu wa wilaya ya Butiama Moses Kaegele ameahidi kwa Dkt. Kiruswa kukutana na uongozi wa mgodi huo ili kujadili changamoto zilizopo ukiwepo ya tozo ya shilingi 1000 inayotozwa na Halmashauri kwa kila mfuko wa mawe.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi mkoa wa Mara Mjiolojia Mayigi Makolobela amewataka wachimbaji katika mgodi huo kufuata Sheria zilizowekwa na Serikali ili kufanya shughuli za uchimbaji kwa tija. Pia, kuwa waaminifu na kuboresha maeneo yanayozunguka mgodi kwa ajili ya usalama wao.

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akipokea maelekezo katika mgodi huo.

Awali, Meneja wa Mgodi wa Irasanilo Gold Mine Isaya Daudi ameongeza kuwa, mgodi umesaidia katika miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo ujenzi wa shule Buhemba. Aidha, mgodi umetoa ajira 77 za moja kwa moja, na wachimbaji zaidi ya 4000 wanaofanya kazi katika mgodi huo.

Young Africans yaifuata Namungo FC
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Decemba 5, 2022