Hatimaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo imemtangaza Dkt. John Pombe Magufuli wa CCM kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwashinda wagombea wengine saba wa vyama vya upinzani.

Akitangaza matokeo hayo jioni hii, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva ameeleza kuwa Dkt. John Magufuli ampata ushindi wa kura 8,882,935 ambazo ni sawa na asilimia 58% ya kura zote zilizohesabiwa, huku akimuacha kwa mbali mpinzani wake mkubwa, Edward Lowassa aliyepata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97% ya kura zote. Mgombea urais kwa tiketi ya ACT – Wazalendo, Anna Mghwira yeye alifanikiwa kupata asilimia takribani 0.65% ya kura zote.

Kufuatia matokeo hayo, aliyekuwa mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu amechaguliwa kuwa Makamu wa rais, akiwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu kuanzishwa kwa taifa la Tanzania.

Kufuatia ushindi huo, NEC inatarajiwa kumkabidhi cheti maalum cha ushindi Dkt. John Magufuli, kesho majira ya saa nne asubuhi katika ukumbi wa Diamond Jubilee.

Hata hivyo, Chadema wameendelea kushikilia msimamo wao wa kupinga matokeo hayo na hawakushiriki katika zoezi la kutangazwa mshindi hivyo hawakusaini fomu maalum zilizotolewa na Tume.

Akiongea baada ya matokeo ya urais kutangazwa, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliwashukuru wa wananchi waliowaamini na kumchagua mgombea wao kwa kura nyingi na kuahidi kuwatumikia na kutekeleza ilani ya chama chao.

“Nawashukuru watanzania kwa kutupa ushindi huu mkubwa na mzuri, na tunawaahidi tuna kazi kubwa ya kutekeleza ilani ambayo ni ahadi tuliyowapa watanzania,” alisema Kinana.

Zanzibar Shwari, Maalim Seif Atangaza Hatua..Hiki Ndicho Kinachoendelea
Juma Duni Awasilisha NEC Pingamizi