Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa marekebisho ya Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2018, hayawazuii wadau wa takwimu kutoa takwimu kwa ajili ya matumizi yao, bali marekebisho hayo yanaweka  misingi ya kuzingatiwa wakati wa utoaji wa takwimu hizo.

Ameyasema hayo alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha (IMF) anayewakilisha Tanzania na nchi nyingine (Africa Group 1 Constituency), Maxwell Mkwezalamba, katika Mikutano ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) mjini Bali Indoneshia.

Amesema kuwa lengo la marekebisho ya sheria hiyo ni kurahisisha ufanyaji wa tafiti na utoaji wa matokeo ya tafiti na sio kuwabana wadau katika ukusanyaji wa taarifa za kitakwimu au kuzuia mijadala ya uchambuzi wa kisera wa matokeo ya takwimu rasmi.

“Tumekubaliana kutumia fursa ya kuboresha Kanuni za Takwimu kwa ajili ya kuweka mazingira ya utekelezaji mzuri  wa vipengele vya sheria vilivyorekebishwa kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kuelewa lengo la marekebisho hayo,” amesema Dkt. Mpango.

Aidha, amesema kuwa marekebisho hayo ya kanuni za takwimu yatawezesha utekelezaji mzuri wa vifungu vya sheria vilivyorekebishwa ambapo ametoa wito kwa wadau kushiriki katika mchakato wa marekebisho hayo.

Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga, amesema kuwa BoT imeendelea kuboresha Sera ya Fedha ya Mwaka 2017 ili kutatua changamoto za Sekta ya Fedha zinazoibuka zikiwemo za uhaba wa mikopo hasa katika Sekta binafsi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha (IMF) anaeiwakilisha Tanzania, Maxwell Mkwezelamba, ameipongeza Tanzania kwa hatua mbalimbali za maendeleo ya uchumi kwa kuwa imeendelea kuwa nchi inayopiga hatua kubwa ya maendeleo na kuwa mfano katika nchi za Afrika.

 

Manara mbaroni sakata la Mo kutekwa
Dkt. Bashiru: Vyama vya siasa nchini havina nidhamu