WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amewaonya wafanyabiashara wote wanaokwepa matumizi ya mashine za kielektroniki kwaajili ya kukusanyia kodi ya Serikali-EFDs na kuwataka kuacha mchezo huo mara moja.

Dkt. Mpango ametoa onyo hilo mjini Dodoma mara baada kufanya ziara ya kushtukiza katika mitaa mbalimbali yaDodoma mjini ya ukaguzi wa wafanyabiashara wa mafuta na kuwabaini wale ambao sio waaminifu.

Aidha, Dkt. Mpango ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Mkoa wa Dodoma kuwapeleka ofisini kwake mawakala wote mkoani humo wanaosambaza mashine za kieletroniki za kukusanyia mapato EFDs baada ya kubaini kuwa zaidi ya mashine 100 zimeharibika na hazitumiki tangu jana.

“Kuna kitu sikielewi na hakiingii akilini, inakuwaje mashine ziharibike kwa kiwango hicho, mashine 100 kuharibika kwa siku mbili ni nyingi na ina maana nimekosa mapato mengi” amesema Dkt. Mpango.

Vile vile amewataka mawakala wote wanaosambaza ama kuuza mashine hizo wakutane naye ofisini kwake mjini humo ili kubaini tatizo na kuongeza kuwa haiwezekani wafanyabishara walipie mashine hizo zaidi ya mwezi uliopita lakini hawapelekewi hali inayozidi kuikosesha Serikali mapato yake.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wamepongeza uamuzi wa Serikali wa kulivalia njuga suala la kodi na kwamba wako tayari kuiunga mkono Serikali kwa kutoa risiti wanapouza bidhaa na kudai risiti zenye viwango sahihi vya manunuzi waliyoyafanya ili kuijengea Serikali uwezo wa kuihudumia jamii.

 

Mke wa Mugabe ampa changamoto mumewe, amtaka ataje jina…
Video: Makonda agawa Computer katika manispaa za jiji la Dar