Serikali imeahidi kutatua kero mbalimbali zinazolikabili Shirikisho la Masumbwi Tanzania (BFT) katika eneo la kufanyia mafunzo pamoja na ofisi pia changamoto mbalimbali zinazolikabili shirikisho hilo.

Hayo ymesemwa mapema hii leo jijini Dar es salaam  na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alipokutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi na wajumbe mbalimbali wa shirikisho hilo ikiwa ni sehemu ya kutambua utendaji kazi wao na changamoto zinazowakabili ili ziweze kutatuliwa.

Amesema kuwa kutokana na tatizo la ukosefu wa eneo rasmi la ofisi na sehemu ya kufanyia mafunzo, yeye atawasiliana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ili kuona namna gani wanaweza kupata eneo kwa ajili ya kulisaidia shirikisho hilo.

“BFT jitahidini muwe na ushirikiano wa karibu na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na msifanye mambo yenu kimya kimya, muwasiliane kwa karibu na BMT kwani hii itasaidia Wizara kushughulikia kero zenu mbalimbali kuliko mkichelewa kutoa taarifa mapema”, amesema Dkt. Mwakyembe.

Aidha, amewahakikishia kuwa, yupo tayari kutafuta wafadhili ndani na nje ya nchi ili waweze kulisaidia shirikisho hilo kutatua kero za uhaba wa vifaa, rasilimali fedha pamoja na ukosefu wa mafunzo kwa makocha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo amelitaka shirikisho hilo kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Serikali ikiwemo kujenga tabia ya ulipaji kodi, kuwaelimisha Wanamasumbwi kuachana na tabia chafu wanapokuwa michezoni pamoja na kuachana na kujihusisha na madawa ya kulevya.

Hata hivyo, Viongozi wanaounda shirikisho hilo pamoja na wajumbe kwa pamoja wamemuahidi Dkt. Mwakyembe na Wizara kwa ujumla kuzingatia masuala mbalimbali ikiwemo kuboresha suala la mawasiliano kati ya Shirikisho na Wizara, kufuatilia suala la mikataba mbalimbali na uwajibikaji yakinifu.

Taasisi za umma zabanwa kuhusu matumizi ya kuni
Uchaguzi Mkuu TAFCA Agosti 10, 2017