Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka vijana kuthamini michezo kwakuwa michezo kwa sasa imekuwa ni ajira ya kudumu ambayo inaweza kubadilisha maisha na kuwapatia vipato vikubwa.

Ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam alipokuwa akikabidhiwa bendera ya taifa na Vijana walioshiriki mashindano ya Shirikisho la michezo la Afrika Mashariki (FEASSSA) yaliyofanyika mwaka huu katika mji wa Gulu nchini Uganda.

“Nataka kuwadhitibishia Watanzania kwamba tutaenzi daima michezo ya UMITASHMITA na UMISETA maana vipaji ndiyo vinapoanzia, niwapongeze sana vijana kwa kushinda medali,  muendelee na juhudi hizo hizo ili muweze kushiriki katika mashindano ya kimataifa yakiwemo Olimpiki, vile vile nawasihi vijana wote kuithamini michezo kwani kwa sasa imekuwa ni ajira ya kudumu,”amesema Dkt. Mwakyembe

Dkt. Mwakyembe amewaasa vijana hao wasithubutu kutumia njia zisizo halali ili kushinda, bali wajitume katika mazoezi na wawe na nidhamu ya hali ya juu kwani michezo ni ajira ya uhakika kwa vijana wengi sio tu Tanzania bali hata katika mataifa yote ulimwenguni.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali imejipanga mwaka ujao kuongeza idadi ya washiriki katika mashindano yatakayofanyika Rwanda na amewasisitiza vijana pamoja na walimu wa michezo mashuleni kuendelea kuwalea vijana na kuibua vijana wengi ili kukabiliana na na tatizo la upungufu wa ajira kwani michezo imekuwa ajira ya uhakika duniani.

Katika michezo hiyo Tanzania imepata medali 10, kwa upande wa riadha na mchezo wa kupokazana vijiti na kushika nafasi ya tatu, lakini pia imeshika nafasi ya tatu kwa upande wa mashindano ya mpira wa miguu kwa wasichana na kuishia hatua ya robo fainali kwa upande wa timu ya wavulana.

 

Amber Lulu atiwa mbaroni kwa makosa ya kimtandao
RC Tabora awaweka kikaangoni Wakurugenzi