Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) katika kuhakikisha amana zote za wanachama zinasimamiwa ipasavyo.

Mwinyi amesema hayo leo katika hotuba yake ya ufunguzi wa jengo jipya la “Hifadhi Building”  la (ZSSF) lililoko Tibirinzi, Wilaya ya Chake Chake , Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo pia, Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad alihudhuria.

Katika hotuba hiyo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha inachukua hatua zinazofaa na kwa wakati katika kuhakikisha mfuko huo unaendelea kuimarika, unaongozwa na kusimamiwa na viongozi walio makini na wanaojiepusha na vitendo vya ubadhirifu, rushwa na wizi.

Amesisitiza kwamba Serikali itahakikisha wanachama wa Mfuko huo wanaishi bila ya kuwa na wasiwasi wa hatma ya amana wanayowekeza ambayo mara nyingi huwa ni tegemeo kubwa katika maisha ya wafanyakazi baada ya kustaafu.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amewataka viongozi kuhakikisha kwamba fedha inayowekezwa inazalisha na shughuli zote za uendeshaji wa taasisi hiyo zinafanywa kwa weledi, umahiri na umakini mkubwa.

Dkt. Mwinyi pia amesisitiza kwamba uongozi ni lazima kila wakati uhakikishe kwamba idadi ya fedha zinazohitajika kulipa stahiki za wananchama wanaostaafu na mafao mbali mbali zinakuwepo kila wakati bila ya nenda rudi na usambufu wa aina yoyote ile.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 6, 2021
Australia yasema Assange yuko huru kurejea nyumbani