Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amezindua Utalii wa Faru katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo Wilayani Same, Kilimanjaro, huku akihamasisha Mamlaka ya wanyamapori kuhamisha baadhi ya Nyumbu waliopo kwenye hifadhi ya Serengeti kuletwa Mkomazi ili kukidhi haja ya wageni.

Aidha Waziri Dk Ndumbaro amesema Hifadhi ya Mkomazi ni muhimu ingawa ina changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya wanyama na binadamu na kuagiza Mamlaka zinazohusika kuhakikisha mabwawa yanachimbwa mara moja ili wanyama wasiende umbali mrefu kutafuta maji.

” Tunataka kuongeza idadi ya watalii kufika Milioni 5 ifikapo mwaka 2025 na kupata mapato yatokanayo na utalii kiasi cha Sh Bilioni 6 kutoka kiasi cha Sh Bilioni 2.6 kwa sasa,”Amesema Dk Ndumbaro.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Same, Edward Mpogolo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu Utalii huo huku akisema anaamini utachochea ukuaji wa uchumi wa Same.

Hali kadhalika Uzinduzi huo umeshuhudiwa na Naibu Waziri wa Maliasili, Mary Masanja, RC wa Tanga, Adam Malima na DC wa Same, Edward Mpogolo.

Wananchi waonywa matumizi mabaya ya ardhi
Simba Queens yaangukia Kundi A CECAFA