Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dkt. Wilbrod Slaa na aliyekuwa mbunge wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu wameingia kwenye mzozo baada ya Dkt. Slaa kuwalalamikia wapinzani kwa kuichafua nchi.

Dkt. Slaa amesema kuwa tuhuma za wapinzani zinazoelekezwa kwa serikali na vyombo vyake kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kwamba imeua demokrasia, vimeichafua serikali kwa kiasi kikubwa.

Ameyasema hayo juzi jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi za kusini mwa Afrika SADC, ambapo Dkt. Slaa alisema kuwa kitendo hicho kinachofanywa na wapinzani si cha kizalendo.

Akijibu madai hayo ya balozi Dkt. Slaa, Lissu amesema kuwa balozi huyo anakanusha kazi yake mwenyewe ya kuikosoa serikali aliyoifanya kwa zaidi ya miaka 20 akiwa mbunge na kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Aidha, Lissu ambaye yuko nchini Ubelgiji akimalizia matibabu yake amesema kuwa hamshangai balozi Dkt. Slaa kwani anatetea kile anachokiamini na anachokifanyia kazi.

”Tatizo alilonalo Dkt. Slaa kwasasa ni rekodi yake ya kusimamia ukweli katika nchi yetu kwa miaka yote aliyokuwa upinzani, chochote anachosema na atakachosema sasa atakuwa anakula matapishi ya mambo yote aliyoyasema na kuyafanya akiwa mbunge na kiongozi wa Chadema,”amesema Lissu

Hata hivyo, Lissu ameongeza kuwa Dkt. Slaa alipata umaarufu kutokana na kazi aliyoifanya akiwa mbunge ya kuikosoa serikali huku akiibua kashfa kubwa za ufisadi zilizotikisa nchi na kusababisha baadhi ya mawaziri kujiuzulu.

Raia waandamana mbele ya Ofisi ya Rais Tshisekedi
Ushahidi wa video kesi ya vigogo wa Chadema watumika rasmi mahakamani