Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa alipata mshangao (surprise) baada ya kusikia uteuzi wa Dkt. Wilbroad Slaa kuwa Balozi.

Profesa Lipumba ambaye aliungana na Dkt. Slaa katika harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kuitosa ngome ya Ukawa ambayo yeye ndiye muasisi wake, amesema kuwa hakuutegemea uteuzi huo.

“Imekuwa kama surprise, sikutegemea kama Dkt. Slaa atateuliwa kwa sababu muda mwingi yuko Canada,” Dk. Slaa anakaririwa na Mwananchi.

“Narudia tena sikutegemea lakini naamini nchi yoyote ambayo Dkt. Slaa atapangiwa atafanya kazi kwasababu najua ni mchapakazi,” aliongeza.

Dkt. Slaa ambaye alitangaza kuihama Chadema muda mfupi baada ya chama hicho kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea urais akiungwa mkono na Ukawa, aliteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli kuwa Balozi anayesubiri kupangiwa kituo cha kazi.

Uteuzi huo ulikuja siku chache baada ya Dkt. Slaa kuhojiwa na vyombo vya habari na kueleza kuwa anafanya kazi katika moja kati ya maduka makubwa nchini Canada ili aweze kujipatia kipato.

 

Kenyatta amualika Raila sherehe za kuapishwa, Raila apanga yake
Magazeti ya Tanzania leo Novemba 25, 2017