Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Jim Yonaz amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka kompyuta 100 na vifaa vingine zikiwemo printa 10, vilivyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 220.
 
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi na kushuhudiwa na baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Umma, Wakuu wa shule na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bariadi.
 
Akikabidhi kompyuta hizo Dkt. Yonaz amewapongeza viongozi mkoani Simiyu kwa kuendelea kufanya ubunifu katika masuala mbalimbali yanayouwezesha mkoa kukua katika nyanja mbalimbali hususani katika uchumi na elimu.
 
“Ninaamini kompyuta hizi zitawasaidia sana wanafunzi hawa na walimu pia yapo mambo yatakayotatuliwa kupitia kompyuta hizi, ili tuweze kuleta elimu bora, tutengeneze wasomi wazuri ambao watachangia katika uchumi wa Taifa letu,”amesema Dkt. Yonaz.
 
Akipokea kompyuta hizo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ameshukuru kwa msaada huo huku akibainisha kuwa lengo la Mkoa ni kuwa mkoa ambao uko kiganjani ambao taarifa yoyote inaweza kupatikana muda wowote.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF, Mhandisi. Peter Ulanga amesema UCSAF kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao inaandaa mpango wa kutoa mafunzo kwa Maafisa TEHAMA ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kibunifu.
 
Kompyuta hizo pamoja na vifaa vingine vimekabidhiwa kwa baadhi ya Wakuu wa Taasisi, Ofisi za wakuu wa Wilaya, Ofisi ya mkuu wa mkoa na baadhi ya wakuu wa shule za Sekondari mkoani humo.

Halmashauri Kuu CCM Taifa (NEC) yawapongeza viongozi mkoani wa Simiyu
Wakulima watakiwa kuacha Kilimo cha mazoea