Timu ya Dodoma Jiji FC inayoshiriki Ligi Daraja ya Kwanza (FDL) imerejea kilele mwa msimamo wa Kundi A baada kupewa ushindi wa pointi tatu na goli tatu katika mchezo wao dhidi ya wenyeji Mlale FC uliovunjia dakika ya 25 baada ya mashabiki wake kumshambulia mwamuzi huku Dodoma ikiwa mbele kwa goli 2-0.

Alama walizopewa Dodoma sasa zinawafanya kufikisha pointi 42 sawa na Ihefu lakini wakiwazidi idadi ya magoli ya kufunga na kufungwa.

Katika maamuzi yaliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almas Kasongo yameweka wazi kuwa, Mlale FC imepoteza mchezo huo kwa kosa la washabiki wake kumshambulia mwamuzi wa kati na mwamuzi msaidizi namba mbili na kusababisha mchezo kuvunjika kutokana na maumivu waliyoyapata waamuzi hao na kuhofia usalama wao huku adhabu hiyo ikitolewa kwa kuzingatia kanuni ya 43(4) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa Klabu.

Amesema, Dodoma imepewa ushindi wa pointi tatu na magoli matatu kwa uzingativu wa kanuni ya 29 (1) ya Ligi daraja la kwanza kuhusu kuvuruga mchezo.

Pia Mlale imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la washabiki wa timu yake kuleta vurugu zilizosababisha kuvunjika kwa mchezo na adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa Klabu.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Rashid Mpenda amefungiwa miezi sita na faini ya shilingi laki tatu (300,000) kwa kosa la kumshambulia mwamuzi wa kati na mwamuzi msaidizi namba mbili kwa kuzingatia kanuni ya 41(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa viongozi.

Pia uwanja wa Majimaji umefungiwa uwepo wa mashabiki katika mechi zote zitakazochezwa katika uwanja huo mpaka pale utakapoboresha ulinzi uwanjani hapo.

Adhabu hii imetolewa kutokana na vurugu iliyotokea ya kushambuliwa kwa mwamuzi hadi mchezo kuvunjika hali ambayo inatishia usalama na amani wakati wa mchezo katika uwanja huo .

Kamati pia imevitaka vyama vya soka vya mikoa kutimiza jukumu lao la msingi la kuratibu na kusimamia ulinzi na usalama viwanjani ili kuepusha vurugu zinazoweza kutokea wakati wa michezo ya ligi mbalimbali.

Baada ya maamuzi hayo, uongozi wa Dodoma kupitia kwa Katibu wake, Fortunatus John wameipongeza Bodi kwa kutenda haki na kudai kuwa maamuzi hayo sasa yamewaongezea morali kuelekea kwenye mchezo wao wa kesho dhidi ya wenyeji Majimaji.

Amesema, mchezo huo pamoja na mechi nyingine ziilizobaki kwao ni muhimu sana kwani wanazihitaji pointi tatu kwa udi na uvumba ili kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Kundi A.

“Kwanza tunaishukuru Bodi kwa kufanyia kazi haraka jambo hili na kutoa maamuzi ya haki ikiwemo kufungai mashabiki ambao walitufanya kuona usalama wetu ni mdogo uwanjani, hivyo maamuzi haya sasa yametuongezea morali ya kupambana katika mchezo wetu wa kesho kwani lengo letu ni kuchukua alama tatu katika mechi zote zilizosalia ili kujihakikishia nafasi ya kupanda daraja,” amesema Katibu huyo.

Tanzania kuisaidia Burundi kujiunga SADC
TPLB: Tutakabidhi ubingwa VPL kwa utaratibu