Uongozi wa Dodoma Jiji umefunguka kuwa mchezo wao dhidi ya Polisi Tanzania kwao wanauchukulia kama Fainali kwa kuwa ndiyo utaamua hatma yao msimu huu.

Dodoma kesho Jumapili (Machi 12) watakuwa wenyeji wa Polisi Tanzania kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara itakayopigwa Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma.

Afisa Habari wa Dodoma Jiji FC Moses Mpunga amesema kila mchezaji wao anatambua umuhimu wa mchezo huo, na wamejiandaa kupambana hadi tone la mwisho, ili kuondokana na mtazamo wa kuwa miongoni mwa timu ambazo huenda zikashuka msimu huu.

“Huu mchezo ni muhimu sana kwetu kwa sababu itatoa taswira yetu msimu huu kutokana na nafasi mbaya tuliyopo katika msimamo wa ligi.”

“Kwenye mchezo huu tutawakosa nyota wetu watatu ambao ni Christian Zigah, Jimmy Shoji pamoja na Steven Sey ambao wanasumbuliwa na majeraha.”

“Polisi ni wapinzani wagumu sana hivyo mchezo huu utakuwa ni wa kufa na kupona lakini sisi tumejiandaa na tutahakikisha kuwa tunaibuka na ushindi ambao ni muhimu sana kwetu.” amesema Moses Mpunga

Hadi sasa Dodoma Jiji FC inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 24, huku Polisi Tanzania ikiwa nafasi ya 15 ikijikusanyoa alama 19.

Ahmed Ally ahimiza umoja na mshikamano Simba SC
US Monastir yaandaliwa mkakati mzito Dar