Mshambuliaji wa klabu bingwa nchini Italia Juventus FC Douglas Costa, amewaomba radhi mashabiki wa klabu hiyo, kwa kosa la kutolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa ligi dhidi ya Sassuolo uliochezwa jana jumapili.

Mshambuliaji huyo kutoka nchini Brazil aliadhibiwa kwa kuonyeshwa kadi nyekundu, baada ya kuthibitika alimtemea mate sehemu za usoni mchezaji wa Sassuolo Federico Di Francesco.

Mwamuzi alifikia maamuzi ya kumuadhibi mshambuliaji huyo, baada ya kufuatilia picha za televisheni na kujiridhisha ni kweli Costa alitenda kwa makusudi, hivyo maamuzi ya kumuonyesha kadi nyekundu yalikua sahihi.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, amewaomba radhi mashabiki wa Juventus FC kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kuandika: “Ningependa kuomba radhi kwa kilichotokea katika mcheazo wetu dhidi ya Sassuolo, najua mashabiki mtakua mmechukizwa na tabia niliyoionyesha, nimejutia na ninawaahidi sitorudia tena.”

“Pia ninaomba radhi kwa wachezaji wenzangu, ambao walikua nami wakati wa mapambano ya mchezo huo kabla sijaadhibiwa. Najua niliwavunja nguvu kwa kiasi fulani, lakini walipambana hadi kufikia hatua ya kumaliza mchezo kwa ushindi.”

“Nimeweka wazi kwa kuonyesha ninalikubali kosa langu, ninatarajia msamaha kwa wote niliowaomba radhi.”

Katika mchezo huo ambao Juventus walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja, mshambuliaji mpya wa mabingwa hao Cristiano Ronaldo alifunga bao lake la kwanza tangu msimu wa ligi ya Italia ulipoanza mwezi uliopita.

Ronaldo amefunga bao hilo, baada ya kuwa kwenye wakati mgumu wa kuzungumzwa na vyombo vya habari, ambavyo vilionyesha kutopendezwa na mwenendo wake tangu alipojiunga na Juventus FC akitokea kwa mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid.

Bodi ya ligi kufanya uchaguzi
TFF yaingilia uchaguzi wa Simba SC