Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) imekataa kuhudhuria mkutano unaotarajiwa kufanyika leo na Umoja wa Mataifa (UN), nchini Geneva Uswizi ukiwa na lengo la kuchangisha fedha za kukabiliana na majanga yanayotokea nchini humo.

Ambapo Mashirika ya misaada yamesema kuwa zaidi ya watu milioni tano wametoroka makazi yao kutokana na ghasia, mapigano, njaa na ukosefu wa utulivu na kwamba maelfu ya raia wa Congo wamelazimika kutafuta hifadhi magharibi mwa Uganda.

Mkutano huo umedhamiriwa kuchangisha dola bilioni 1.7 kupunguza majanga hayo kwa watu waishio nchini Congo.

Mpaka sasa serikali ya DRC haijajibu mwaliko wa Umoja wa mataifa ikisema taasisi hiyo kuu imetilia chumvi hali halisi nchini na ukubwa wa tatizo liliopo.

Wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu ndani ya DRC wamezusha wasiwasi kutokana na hatua hiyo ya serikali kususia mkutano huo mkuu mjini Geneva.

Aidha Mashirika ya misaada yanasema kuwa DRC kwa sasa inakabiliwa na majanga ambayo yamesababisha watu zaidi ya milioni 3 kuhitaji msaada, miongoni mwao watoto milioni 2 wakiwa wanaugua utapia mlo, na watu milioni 4.5 wamepoteza makazi yao.

 

 

 

Wamiliki wa mitandao ya kijamii watakiwa kujisajili
Mhagama awataka viongozi wa dini kuliombea taifa