Chama cha Waajiri Afrika Mashariki (EAEO) kimesema nusu ya wahitimu wa vyuo vikuu katika nchi za ukanda huo hawana sifa na ujuzi wa kuajiriwa.

Hayo yamezungumzwa katika mkutano wa chama na Dk Aggrey Mlimuka pamoja na Mwenyekiti wake Rosemary Ssenabulya, ambao wamesema ni muhimu tatizo la kukosa sifa za kuajiriwa kwa wahitimu hao lifanyiwe kazi na wadau wote.

Mlimuka amesema katika tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa vyuo vikuu na vya kati katika nchi zote za Afrika Mashariki vinatoa elimu ambayo inawafanya vijana washindwe kuajiriwa.

Amesema ili kukabiliana  na tatizo hilo lazima vyuo viandae vyema wahitimu kwa kuwapa uhusiano baina ya mitaala na masomo na mahitaji katika soko la ajira.

”Nilimsikia Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa akieleza jambo hili napenda kueleza tatizo hili lipo katika nchi zote, lazima sasa mafunzo ya vyuo yajibu changamoto sehemu za kazi na kuwapa ujuzi wahitimu” amesema Mlimuka.

Amesema ni lazima vijana wapewe elimu itakayowawezesha kujiajiri wenyewe mara baada ya kuhitimu mafunzo katika ujuzi mbalimbali.

Aidha Ssenabulya amedai kuwa tatizo la ukosefu wa ujuzi limekuwa likiwaathiri zaidi waajiri sababu wao ndio wanaotafuta wafanyakazi kutoka nje ya Afrika Mashariki wenye uwezo kwa gharama kubwa.

Imebainishwa kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 60,000 wanahitimu vyuo vikuu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda , Rwanda, Burundi na Sudan Kusini na nusu ya wahitimu hao hawana vigezo vya kuajiriwa.

 

Kocha Taifa Stars atamba kuibuka na ushindi dhidi ya DR Congo, kesho.
Thomas Tuchel kumvua ukocha Arsene Wenger