Chama cha soka nchini Argentina (AFA), kimemtangaza Edgardo Bauza, kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo.

AFA, wamefikia hatua ya kumtangaza kocha huyo baada ya kumaliza suala la kuvunja mkataba wake na klabu ya Sao Paulo ambayo alikua anaitumikia katika nchi jirani ya Brazil.

Bauza anachukua nafasi ya Gerardo Martino, ambaye alishindwa kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa fainali za mataifa ya kusini mwa Amerika (Copa America) miezi miwiwli iliyopita, kufuatia kufungwa na Chile kwa changamoto ya mikwaju ya penati.

Mwenyekiti wa chama cha soka nchini Argentina, Armando Perez amemthibitisha kocha huyo katika mkutano na waandishi wa habari na kueleza kwamba wana matumaini makubwa ya kupata mafanikio chini yake.

Hata hivyo Bauza mwenye umri wa miaka 58, bado hajawasili nchini Argentina, kwa ajili ya kutambulishwa rasmi.

“Tumefikia maamuzi ya kumtangaza Bauza kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa, na tunaamini ataweza kufanikisha malengo yanayokusudiwa katika soka la nchini Argentina,” Alisema Armando Perez

“Anatarajiwa kuwasili Argentina mwishoni mwa juma hili na tutamalizanae kwa kila jambo, ili aanze kazi yake haraka iwezekanavyo.” Aliongeza Perez

Bauza, mwenye umri wa miaka 58, aliwahi kupata mafanikio akiwa mchezaji wa klabu za Rosario Central na Independiente za nchini Argentina, Junior de Barranquilla (Colombia) pamoja na Veracruz (Mexico).

Kwa upande wa nafasi ya ukocha, Bauza amewahi kuziongoza klabu za Liga Deportiva de Quito(Ecuador) na San Lorenzo (Argentina) kushinda taji la ligi ya mabingwa Amerika ya kusini (Copa Libertadores) mwaka 2008 na 2014.

Wakati huo huo gwiji wa soka nchini Argentina Diego Maradona, ameonyesha kufurahishwa na uteuzi wa kocha huyo kwa kusema kikosi cha timu yake ya taifa kimepata mtu sahihi, ambaye ataweza kufikia malengo yanayokusudiwa kila kukicha.

Kikosi cha Argentina kinatarajiwa kuanza kampeni ya kusaka nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, kwa kupambana na Uruguay Septemba mosi mjini Mendoza.

Young Africans Waitwa Kwenye Mkutano Mkuu
Nay wa Mitego: Tumemalizana na BASATA, 'Pale Kati' itaanza kuchezwa