Aliyekua mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Senegal El-Hadji Diouf amefichua siri ya baadhi ya wachezaji waliowahi kujiunga na Liverpool wakati wa utawala na nahodha Steven Gerrard kushindwa kufurukuta huko Anfield.

Diouf ambaye alimalizia soka lake akiwa na klabu ya Sabah FA ya nchini Malaysia mwaka 2015, amefikia hatua ya kufichua siri hiyo,baada ya kuumizwa na kitendo cha kuondoka kwa mshambuliaji Mario Balotelli ambaye alijiunga na klabu ya Nice ya Ufaransa kama mchezaji huru.

Diouf amesema alimuonya Mario Balotelli juu ya kujiunga na Liverpool kwa sababu nahodha wa kipindi hicho Steven Gerrard alikua ni mtu mwenye wivu.

Balotelli alijiunga Liverpool mwaka 2014 kwa ada ya Pauni milioni 16. Balotelli aliwahi kusema maamuzi yake ya kujiunga na Liverpool ndio yalikuwa maamuzi mabaya zaidi katika maisha yake.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, alifunga mabao mawili  dhidi ya Marseille katika mchezo wake wa kwanza katika ligi ya Ufaransa mwishoni mwa juma lililopita.

Image result for el Hadji Diouf 2016El-Hadji Diouf (Kulia) alipokua Blackburn Rovers akibishana na Steven Gerrard wakati akiitumikia Liverpool FC.

Diouf aliliambia gazeti la L’Equipe: “Nilimwambia asiende Liverpool, haikuwa sehemu yake kwa sababu vitu visingeenda sawa na Gerrard,”

“Gerrard ni mtu mwenye wivu ambaye hapendi wanaume wenye vipaji na mvuto wawe sambamba na yeye. Mario ni mtu mzuri na anafaa kusikilizwa, sio mtu anayeweza kusababisha matatizo kwenye vyumba vya kubadilisha nguo .” alisema Diouf.

Hata Hivyo Gerrard ambaye alianza kuitumikia Liverpool tangu akiwa na umri mdogo, alilazimika kuondoka Anfield mwaka 2015 na kutimkia nchini Marekani ambapo kwa sasa anaitumikia klabu ya LA Galaxy.

Kumekucha: TFF Yataja Makundi Ligi Daraja La Pili
Marekani yaweka vitisho Korea Kusini, Ndege za kivita zapaa angani