Mshambuliaji wa klabu ya Mbeya City, Eliud Ambokile amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/2019.

Ambokile ametangazwa hii leo katika mkutano wa waandishi wa habari, uliofanyika makao makuu ya shirikisho la soka nchini (TFF), na kuongozwa na afisa habari wa shirikisho hilo, Clifford Mario Ndimbo.

Ndimbo amesema Ambokile ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Ibrahim Ajibu wa Yanga na Stamili Mbonde wa Mtibwa Sugar alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL.

Tuzo hiyo mara ya kwanza kwa msimu huu ilichukuliwa na straika wa Simba, Meddie Kagere baada ya kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City.

Wakati huo huo kamati ya Tuzo za Wachezaji Bora Ligi Kuu Tanzania Bara, imeanzisha tuzo mpya ya Kocha Bora wa mwezi itakayokuwa inatolewa kila mwezi kwa lengo la kutambua mchango wa kocha husika katika ligi hiyo.

Ndimbo amesema baada ya kamati kukaa chini na kuanzisha tuzo hizo, ya kwanza imefanikiwa kwenda kwa Kocha wa Mbao, Amri Said akiwa kama Kocha bora wa mwezi Agosti.

Wakati huohuo, kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ametwaa tuzo hiyo akiwa kama Kocha Bora wa Mwezi Septemba.

Kwa mujibu wa TFF, Tuzo hizo ni chachu kwa makocha wote wa Ligi Kuu Bara kama changamoto ya kuhakikisha klabu zao zinafanya vizuri ili kujitengenezea mazingira ya kuwa washindi kila mwezi.

Wimbo wa 'Hela' warejeshwa, Kiba afunguka kisa chake
Naby Keita yupo 'FIT', kurudi Anfield leo

Comments

comments