Wakati mashabiki wa Manchester City na Arsenal wakihesabu saa chache kabla ya kushuhudia mtanange wa timu hizo, kocha wa washika bunduki hao wa London, Unai Emery amempa sifa za kipekee mwenzake Pep Guardiola.

Emery mwenye uzoefu wa kukutana na Guardiola tangu msimu wa mwaka 2008/2009 alipokuwa akikinoa kikosi cha Valencia, amesema kuwa anaamini ni vigumu katika ulimwengu wa sasa wa soka kumpata kocha bora zaidi ya kocha huyo.

Meneja huyo wa Arsenal ana historia ya kutonyakua alama tatu dhidi ya kikosi anachokiaongoza Guardiola mara zote walipokutana.

“Nimeshafanya uchambuzi wa timu nyingi na makocha wengi, lakini nafikiri ni vigumu sana kumpata kocha bora zaidi ya Guardiola,” Emery aliwaambia waandishi wa habari.

“Ujuzi na uzoefu wake kwenye soka ni mkubwa. Tulianza pamoja, alianza na kikosi cha pili cha Barcelona na mimi nilianza na Lorca na Almeria. Nimejifunza mengi kwa kuangalia timu zake. Ni vizuri kuangalia wakufunzi wenzako kwa ajili ya kujifunza vitu tofauti kati yetu. Ninadhani anafanya vizuri zaidi ya makocha wote duniani,” aliongeza.

Amesema kuwa amemuona jinsi alivyotumia mbinu bora kuongoza vikosi vyenye wachezaji wakubwa kama Barcelona, Bayern na Manchester City na kwamba mbinu yake imewabadili wachezaji na kuwafanya wawe na uwezo wa kulipwa fedha nyingi zaidi.

Kesho, Arsenal watasafiri kuelekea kwenye uwanja wa Etihad kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu, huku mashabiki wao wakiwa na matumaini ya kulipa kisasi cha kipigo cha 2-0 walichopata wakiwa jijini nyumbani, Agosti mwaka jana.

Bungeni: Mkurugenzi NEC alivyojitenga na ufisadi wa mabilioni
Video: Mfungwa Aliyesamehewa na Magufuli akutwa na sare za Jeshi

Comments

comments