Mtendaji mkuu wa chama cha soka nchini England (FA), Martin Glenn amesema harakati za kumsaka mbadala wa kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo, huenda zikahusishwa makocha wa kigeni pamoja na wazawa.

Glenn alitangaza mustakabali huo, kufuatia maamuzi ya kujiuzulu yaliyochukuliwa na Roy Hodgson usiku wa kuamkia jana, huko nchini Ufaransa, kufutia kikosi chake kupoteza mchezo wa hatua ya mtoano wa Euro 2016 dhidi ya Iceland, kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.

Glenn alisema ni wakati mzuri kwa FA, kuangalia uwezo wa makocha wengine ambao watakuwa na vigezo tofauti, ili kufanikisha azimio la kuiwezesha England kufikia lengo la kufanya vyema kimataifa.

Alisema wanaamini ni wazi wigo wa ukufunzi umetanuka kwa sasa, na huenda wakafanya makosa endapo watafunga milango kwa makocha wa kigeni kuomba nafasi ya kutaka kuwa warithi wa Hodgson.

“Tutaangalia uwezo wa mtu nasi utaifa, tulipofikia sasa hakuna haja ya kuangalia uzawa wala ugeni,” Alisema Glenn.

Hata hivyo kiongozi huyo aligoma kabisa kuzungumzia mchakato wa kumsaka kocha mpya wa timu ya taifa ya England, ambao utaanza wakati wowote kuanzia sasa, huku akisita kutangaza watu ambao wanawatarajia kuingia katika kinyang’anyiro hicho.

“Sipo hapa kutaja mchakato utakavyokua wala kutaja majina ya watu tunaowatarajia katika hatua hiyo, ila jukumu letu kwa sasa ni kuangalia mwenye vigezio vitakavyokidhi malengo tuliyoyakusudia.” Alisema Glenn.

England itakua na kocha mpya katika harakati za kusaka nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, zitakazofanyika nchini Urusi, na lengo kubwa ni kuhakikisha wanafuzu mtihani huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu.

Katika harakati za kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, England imepangwa katika F lenye timu za Scotland, Slovakia, Slovania, Lithuania pamoja na Malta.

Vincenzo Montella Akabidhiwa Mikoba Ya AC Milan
Unai Emery Avishwa Viatu Vya Laurent Blanc