Timu ya taifa ya England itacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Italia utakaochezwa Machi 27, kwenye uwanja wa Wembley jijini London.

Chama cha soka nchini England (FA), kimethibitisha taarifa za kuchezwa kwa mchezo huo, ambao utakua sehemu ya maandalizi ya kuelekea fainali za mataifa ya Ulaya (Euro 2020).

Mataifa ya England na Italia yamefuzu kucheza fainali hizo, ambazo kwa mara ya kwanza mwaka 2020, zitachezwa kwa mfumo mpya wa kuzunguuka viwanja mbalimbali barani Ulaya.

Kwa mara ya mwisho timu za England na Italia zilikutana miaka miwili iliyopita na zilitoka sare ya bao moja kwa moja.

Katika fainali za Euro 2020, England imepangwa kundi D lenye timu za Croatia, Jamuhuri ya Czech na mshindi atakaepatikana katika michezo ya mtoano ya kufuzu. Italia wamepangwa kundi A na Uturuki, Wales na Uswiz.

Fainali za Euro 2020 zimepangwa kuanza Juni 12, katika viwanja mbalimbali barani Ulaya.

Video: Pazia lafunguliwa, Mufti apiga marufuku madufu moto
New Zealand: Volkano yalipuka kisiwa cha watalii