Beki wa Man Utd Eric Bailly  atakaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi miwili, kufuatia majeraha ya goti aliyoyapata wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England dhidi ya Chelsea mwishoni mwa juma lililopita.

Beki huyo kutoka nchini Ivory Coast amekua muhimili mkubwa katika safu ya ulinzi ya Jose Mourinho tangu alipoanza kuitumikia Man Utd mwanzoni mwa msimu huu, akitokea Villarreal.

Bailly, mwenye umri wa miaka 22, alithibitisha taarifa za uwezekano wa kukaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi miwili katika kurasa zake za mitandao ya kijamii (Facebook na Twitter).

“Ninawashukuru mashabiki wangu wote ambao wamekua wakinitumia ujumbe wa kunitakia pole tangu nilipopata majeraha,”

“Ninatarajia kuonekana tena uwanja baada ya miezi miwili, nitaimiss sana Man Utd pamoja na timu yangu ya taifa. Mwenyezi mungu nisaidie!” Aliandika Bailly.

Beki huyo aliyeigharimu Man Utd kiasi cha Pauni milioni 30 kama ada yake ya uhamisho, tayari ameshacheza michezo tisa ya ligi ya England pamoja na michezo mitatu ya Europa League.

Frank de Boer Awekwa Kiporo Inter Milan
Video: Makonda azindua wiki ya kinga tiba mkoa wa Dar es salaam