Hatimaye mahasimu wa kisiasa waliokuwa kwenye ngome moja ya CCM hapo awali, Mbunge wa viti maalum anaemaliza muda wake, Esther Bulaya na mbunge wa Bunda, Stephen Wasira wamekutana uso kwa uso.

Wawili hao sasa wanakutana wakiwa katika ngome mbili tofauti baada ya Esther Bulaya kuhamia Chadema akiwa na kiu ya kutaka kumuondoa Wassira katika kiti cha ubunge wa jimbo hilo.

Awali, Bulaya alionekana kushindwa kuisogelea ndoto yake baada ya kushindwa kupewa ridhaa ya kugombea kupitia kura za maoni na badala yake kupewa nafasi ya viti maalum kupitia Chadema. Hata hivyo, vita ya wawili hao imeonekana kutoepukika baada ya uongozi wa ngazi ya juu ya chama chake hicho kipya kumteua kuwania nafasi ya ubunge wakiamini yeye ndiye dawa ya Wassira.

Harakati za kuanza mapambano zilianza na changamoto zake hapo jana katika jimbo la Bunda Mjini baada ya Esther Bulaya kwenda kuchukua fomu.

Wasiwasi wa kutaka kuhujumiwa mapema ulianza jana wakati mgombea huyo alipoenda kuchukua fomu katika ofisi za NEC zilizoko mjini Bunda ambapo alizuiwa na kusubirishwa kwa muda mrefu hadi pale wafuasi wa chama hicho walipotishia kufanya fujo baada ya kuona wanasubiri kwa muda mrefu isivyo kawaida.

“Kwanza kabisa kulikuwa kuna mizengwe kidogo. Hata hivyo, lazima maadui zetu wakiona kuna mtikisiko na wanaweza kutoka. Na kwa sababu wanajeuri ya kukaa madarakani, wanafikiri wanaweza kuwaamlia wananchi viongozi wanaowataka wao. Lakini tumeshughulikia tukiwa na mwenyekiti wa chama na katibu wa jimbo na viongozi wengine,” alisema Esther Bulaya baada ya kuchukua fomu hapo jana.

Kwa upande wa Stephen Wassira ambaye pia ni waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika atalazimika kugawanya nguvu zake za kupiga debe kwakuwa amechaguliwa kuwa kati ya timu ya watu 32 wa CCM watakaozunguka nchi nzima kumnadi mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli.

Nani ni nani? Jibu litapatikana Oktoba 25 baada ya wananchi kupiga kura na kutengua kitendawili hicho.

 

Soldado: Nilishindwa Kujiamini
Serikali Yampiga 'Marufuku’ Lowassa Kutumia Uwanja Wa Taifa