Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na wafuasi wengine zaidi ya 10 wamekamatwa na Jeshi la Polisi.

Watu hao wamekamatwa wakati Jeshi hilo la Polisi likiwatawanya kwa mabomua ya machozi wafuasi wa vyama vya upinzani waliohudhuria mkutano wa kumnadi mgombea udiwani kata ya Turwa, (Chadema) ambapo kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alitarajiwa kuhutubia mkutano huo.

Akizungumzia tukio hilo, katibu wa Chadema mkoa wa Mara, Chacha Heche amedai kwamba chama chake kimezuiwa kufanya mkutano wa kampeni kuanzia leo Agosti 8, 2018 hadi Agosti 11.

Aidha, Heche amesema chama hicho hakikupewa barua rasmi ya kuzuiwa kufanya mkutano huu wa kampeni.

“Walikuja asubuhi kwenye ofisi za chama wakitaka tusifanye mkutano lakini hakukuwa na sababu ya msingi ya sisi kutofanya mkutano,” amesema.

Naye Zitto amesema wataendeleza kampeni hizo kwa kushiriki mikutano ya kampeni ya NCCR-Mageuzi.

Zitto pia amedai kuwa Polisi wamemzuia kumuona Esther kituo cha polisi anakoshikiliwa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo zimechapishwa na Mwananchi, zimeeleza kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, Henry Mwaibambe hakupatikana kuzungumzia kamatakamata hiyo wala simu yake ya mkononi haikupokewa.

Tanzia: Mzee Majuto afariki dunia
Video: Kauli ya Viongozi wa Dini baada ya kukutana na Rais Magufuli Ikulu leo