UMOJA wa Ulaya (EU), umeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 18.7 sawa na Shilingi bilioni 44.3 kwa ajili ya Programu ya Kunusuru Kaya Maskini awamu ya pili.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba ameipongeza EU kwa msaada huo na kusema utasaidia kupunguza uhaba wa fedha uliopo kwa ajili ya programu hiyo.

“Lengo la ufadhili huu ni kuwezesha PSSN kuboresha hali za uchumi ya wanawake kwa kufadhili familia masikini kuwawezesha kupata fursa za kuongeza kipato na huduma za kiuchumi na za kijamii,” amesema Katibu Mkuu.

Amesema lengo la PSSN awamu ya pili limefikiwa kwa kiasi kikubwa hasa kwa kuwapatia kazi ya uzalishaji ili kuboresha maisha yao, kuongeza vipato na kuunda rasilimali za kijamii.

Kwa upande wake Mkuu wa ushirikiano wa maendeleo kutoka ubalozi wa Sweden nchini, Sandra Diesel amesema wanatarajia kuongeza ufadhili zaidi ili kupunguza upungufu wa fedha uliopo kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa programu na kufikia malengo.

Katika hatua nyingine Serikali ya Italy imeipatia Tanzania mkopo wa Euro 19,790,400 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 49.1, pamoja na msaada wa Euro 200,000 sawa na Shilingi milioni 496.5, kwa ajili ya kuendeleza taasisi za ufundi za elimu ya juu nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema mradi huo unalenga kuanzishwa kwa vituo vya ujasiriamali, ubunifu na kukuza teknolojia katika taasisi nne za ufundi za elimu ya juu.

Serikali ya Sweden imekuwa ikiisaidia Tanzania katika miradi mbalimbali tangu mwaka 2015 ambapo kupitia mradi huu ilitoa dola za Marekani milioni 86 kwa awamu ya kwanza ya programu na baadae kutoa dola za kimarekani milioni 63.

Serikali yatangaza mfumo mpya wa tozo
Simon Msuva azianika Simba SC, Young Africans