AS Roma wameweka dhamira ya kilipiza kisasi dhidi ya FC Barcelona katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya robo fainali ligi ya mabingwa barani Ulaya, utakaochezwa kesho mjini Roma, nchini Italia.

AS Roma walikandamizwa mabao manne kwa moja katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Camp Nou juma lililopita, na kesho watalazmika kusaka ushindi wa mabao matatu kwa sifuri ili wasonge mbele katika hatua ya nusu fainali.

Meneja wa wababe hao wa Stadio Olimpico Eusebio Di Francesco, amesema anaamini suala la kupata mabao hayo linawezekana huku akikumbushia wakichokifanya katika hatua ya makundi dhidi ya Chelsea waliokubali kipigo cha mabao matatu kwa sifuri, baada ya kuchapwa na The Blues mabao manne kwa moja jijini London.

“Kwa nini isiwezekane? Kwenye soka lolote linawezekana na hatujakatishwa tamaa na matokeo ya mchezo wa mkondo wa kwanza, tumejiandaa kupambana ili na sisi tushinde katika uwanja wetu wa nyumbani,” Amesema Di Francesco.

“Wakati mwingine unaweza kudharaurika kutokana na matokeo ya mchezo wa kwanza, jambo hilo tunalikubali kwa sababu tulifungwa, ila nina wahakikishia hakuna kitakachoshindikana katika mchezo wa kesho.

“Mara kwa mara huwa napenda kuona tunapata matokeo mazuri katika uwanja wetu wa nyumbani.” Alisema meneja huyo kuwaambia waandishi wa habari.

AS Roma tayari wameshacheza hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya mara tatu, na walitolewa mara mbili katika hatua hiyo dhidi ya Manchester United mwaka 2007 na 2008.

Mwaka 1984 waliwahi kupiga hatua katika michuano hiyo ilipokua ikiitwa European Cup, na kucheza mchezo wa fainali, lakini walipoteza dhidi ya Liverpool.

Video: Viongozi waliotelekeza watoto mikononi mwa Makonda
Simba yaikandamiza Mtibwa Sugar, yaendelea kuelea kileleni