Bosi mpya wa kikosi cha klabu ya Arsenal Unai Emery amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na kiungo kutoka nchini Argentina na klabu ya Sevilla ya Hispania Éver Maximiliano David Banega, akimtaka ajiunge naye huko kaskazini mwa jijini London.

Kwa mujibu wa gazeti la Hispania liitwalo Estadio Deportivo, Banega amekua akiwindwa na Unai katika mipango yake ya usajili tangu alipotua Emirates Stadium mwezi uliopita, kwa lengo la kutaka kumtumia katika mfumo wake wa 4-2-3-1.

Unai amedhamiria kumtumia Banega endapo mipango ya kumsajili itafanikiwa, katika sehemu ya kiungo ambayo itakua na wachezaji watatu, wakiongozwa na mshambuliaji mmoja.

Hata hivyo Emery anapewa nafasi kubwa ya kumtwaa mchezaji huyo, kufuatia mazungumzo ya uhamisho wa Banega yaliyokua yakiendelea kati ya uongozi wa Sevilla na Valencia kuvunjika mwishoni mwa juma lililopita.

Gazeti la Estadio Deportivo limeripoti kuwa, wakala wa Banega tayari ameshawasili mjini London kwa lengo la kuanza mazungumzo na uongozi wa Arsenal.

Wakati mipango ya usajili wa Banega ikiendelea, Unai pia amejipanga kumsajili kiungo kinda mwenye umri wa miaka 17 Yacine Adli anaewatumikia mabingwa wa soka nchini Ufaransa (Paris Saint-Germain) na kiungo wa Sevilla Steven N’Zonzi, katika kipindi hiki cha dirisha la usajili.

Tayari bosi huyo wa Arsenal ameshakamilisha usajili wa wachezaji wawili mpaka sasa ambao ni mlinda mlango kutoka nchini Ujerumani Bernd Leno na beki wa pembeni kutoka Uswiz Stephan Lichtsteiner, huku beki kutoka Ugiriki na klabu ya Borussia Dortmund Sokratis Papastathopoulos akitarajiwa kutua klabuni hapo wakati wowote juma hili.

Real Betis yaingilia kati usajili wa Yerry Mina
Majaliwa: Mitandao isitumike kukwamisha shughuli za Serikali